Mpenzi msomaji wa KUKUBATACAMP leo nimetamani tujikumbushe kisa kimojawapo cha zamani kinachusu ndege ya shirika la ndege la Tanzania iliyotekwa nyara na watekaji kushinikiza Mwalimu JK nyerere ajiuzuru sasa endelea.
KUTOKANA na hali ya kisiasa
ilivyokuwa ikiendelea tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika, kuna watu
walioona kuwa hawaridhishwi na Serikali ya Mwalimu Nyerere hasa vijana kiasi
cha kupata ujasiri hata kuteka ndege ya abiria kwa lengo la kuishinikiza Serikali
kufuata matakwa yao. Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Boeing 737,
ilitekwa mjini Mwanza na vijana watano wa Dar es Salaam.
Huo ulikuwa ni utekaji wa kwanza wa
aina yake. Kabla ya hapo kulikuwa na utekaji uliofanywa na Serik
ali ya Tanzania
mara mbili tofauti. Wa kwanza ulikuwa mwaka 1972 na mwingine 1979. Lakini huu
ulikuwa wa kipekee kabisa. Na ingawa ulikuwa wa kisiasa, Serikali ya Tanzania
haikutaka ijulikane hivyo.
Baada ya maagano na ndugu, jamaa na
marafiki, abiria walipanda katika ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania
iliyokuwa na jina la Kilimanjaro, Boeing 737, kwenye uwanja wa ndege wa
Mwanza, Ijumaa ya Februari 26, 1982, saa 11 jioni.
Uwanja wa ndege wa Mwanza ulikuwa na
sifa mbaya kwa sababu haukuwa na usalama kiasi kwamba baadhi ya marubani
walikuwa wakiutaja kama ‘kituo cha basi.’
Makundi yaliyokuwa uwanjani hapo
yalikuwa ya kawaida kama ya siku zote kwa wasafiri wa kwenda Dar es Salaam.
Wasafiri wengi walikuwa ni Wahindi, Waarabu na Waafrika wachache. Ingawa mambo
yote yalionekana kuwa ya kawaida, jambo dogo liliifanya safari hiyo isiwe ya
kawaida.
Ndege ya Kilimanjaro ilipaa angani
kutoka uwanjani hapo saa 11.20 jioni ya siku hiyo kwa kile kilichotazamiwa kuwa
ni safari ya dakika 90 - maili 500, kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam.
Lakini ikageuka kuwa safari ya juma
zima - maili 9,500 - na kwa wakati mwingi abiria wa ndege wakisafiri ‘chini ya
mtutu wa bunduki’ kabla ya kuwasili Dar es Salaam.
Dakika tano tu baada ya ndege kupaa
angani, vijana wanne walisimama ghafla kwa wakati mmoja. Mmoja wao alijipenyeza
ghafla katika chumba cha rubani, halafu akaelekeza ‘bastola’ yake kwenye kichwa
cha mmoja wa marubani wa ndege hiyo, Kapteni Deo Mazula, na kumtaka awapeleke
kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.
Baadaye ilikuja kujulikana kuwa
majina ya watekaji wale ni Musa Memba (25), Mohamed Ali Abdallah (26) na ndugu
yake Abdallah Ali Abdallah (22), Mohamed Tahir Ahmed (21) na Yassin Memba (21).
Kiongozi wao alikuwa Musa Memba.
Wakati huo huo, watekaji nyara
wengine, huku wakipunga ‘bastola’ zilizotengenezwa kwa vigogo vya miti na
‘mabomu’ ya kutupwa kwa mkono, waliwatangazia abiria kuwa wao ni viongozi wa
‘Vijana wa Harakati za Mapinduzi Tanzania’ na kwamba shabaha yao ni
“kuhakikisha kuwa Rais Julius Nyerere anajiuzulu.”
Wakati hayo yakitokea, Rais wa
Tanzania waliyemtaka ajiuzulu, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa Ikulu mjini Dar
es Salaam akijiandaa kurudi nyumbani baada ya kupokea risala kutoka kwa
Chipukizi nchini waliomwahidi kuwa “Tutaendelea kuwa watiifu, wakakamavu na
wenye bidii kwa kuwa tunafahamu mchango wetu unahitajika sana katika ujenzi wa
nchi.”
Mpaka wakati anaondoka kwenda
nyumbani kwake, Msasani, akiwa amefurahishwa na risala aliyosomewa na
Mwenyekiti wa Taifa wa Chipukizi, Frank Uhahula (15) wa darasa la saba katika
Sule ya Mingi ya Tumbi, Kibaha katika mkoa wa Pwani, Mwalimu Nyerere hakuwa
amejua kilichotokea upande mwingine wa nchi -Mwanza.
Watekaji nyara hao waliwaamuru
abiria wote wakae kimya kwenye viti vyao na kufumba macho yao na, kwa sababu
ambazo hazikujulikana lakini za kustaajabisha, waliwalazimisha watumishi kuzima
viyoyozi vya ndege. Wakati hali ya hewa katika ndege hiyo ilipoanza kuwa nzito
na kukaribia kutovumilika tena, ndege hiyo ilitua mjini Nairobi kwenye Uwanja
wa Ndege wa Jomo Kenyatta.
Lakini katika kipindi cha dakika
kadhaa baadaye, Rais Nyerere alipewa taarifa za kutekwa kwa ndege hiyo na
kuambiwa kwamba tayari ilishatua Nairobi, Kenya. Waziri wa Mawasiliano na
Uchukuzi, John Samuel Malecela, ambaye aliteuliwa rasmi kushughulikia utekaji
huo, alitumwa kwenda Nairobi kushughulikia tatizo hilo. Mwalimu Nyerere alitaka
kuwa na hakika kwamba Serikali ya Kenya haingeruhusu ndege hiyo iondoke
Nairobi.
Wakati huo huo polisi wa Kenya
wakifunga uwanja wa Ndege wa Kenyatta, na wanajeshi walisambazwa uwanjani hapo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Robert Ouko, alikuwa uwanjani hapo akitokea
Addis Ababa, Ethiopia, wakati ndege ya Tanzania ilipotua.
Alipopewa habari za yaliyotokea, Dk
Ouko hakusita, alikwenda kwenye chumba cha kuongozea ndege kujaribu
kushughulikia jambo hilo. Akizungumza kupitia katika redio ya ndege hiyo, mmoja
wa watekaji wa ndege hiyo alijitambulisha kwa jina la Luteni Wami, ofisa wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Alisema kuwa ni lazima Rais Nyerere
ajiuzulu vinginevyo ndege hiyo italipuliwa. Dk Ouko alijaribu kujadiliana na
mtekaji huyo, lakini alijibiwa: “Tayari nimeshaua abiria watatu na nitaendelea
kuwaua wengine zaidi.”
Dk Ouko alistushwa na kauli hiyo.
Ilimbidi amsihi mtekaji huyo akimwambia, “Usiendelee kuua zaidi.” Lakini
ukweli wa mambo ni kwamba hakuna mauaji yoyote yaliyokuwa yametokea mpaka
wakati huo.
Kupitia mawasiliano yao ya redio ya
upepo, mtekaji huyo alimwambia Waziri Ouko hivi: “Sasa namuua huyu
rubani.” Rubani mwingine aliyekuwa akisaidiana na Kepteni Deo Mazula ni Oscar
Mwamwaja (kuna vyombo vingine vya habari vya Ulaya vilimtaja kwa jina la
Mwangala Jotham).
Lakini Dk Ouko akamjibu kwa
kumwambia kuwa huo utakuwa ujinga kwa sababu “…rubani huyo atahitajika kuirusha
ndege hiyo kwenda kwingineko.” Mtekaji huyo akajibu: “N’naweza kuendesha ndege
hii mwenyewe. Mimi ni luteni wa anga.”
Watekaji hao walitaka ndege hiyo
ijazwe mafuta kwa ajili ya safari ya kwenda Saudi Arabia. Akiwa hana lingine la
kufanya, Waziri Ouko alikubaliana na matakwa hayo.
Wakati huo huo katika mji wa Dar es
Salaam, kumbukumbu za kijeshi zilianza kuchunguzwa kutafuta jina la Luteni
Wami. Jina hilo halikupatikana popote. Wala hakukuwa na cheo chochote cha
uluteni wa anga katika jeshi la Tanzania.
Ni kitu gani kiliendelea baada ya
hapo? Fuatilia toleo lijalo.
CHANZO: kutoka katika vyanzo mbalimbali katika mtandao
No comments:
Post a Comment