·
Add caption |
Historia ya Rwanda ni ndefu iliyojaa misukosuko ya kisiasa, kupinduana, vita na mauaji ya wenyewe kwa wenye yaliyosababishwa na ubaguzi wa kikabila.
Rwanda imekuwa ikipita katika vipindi vigumu na vya hatari. Vipindi hivi hufuatana na mauaji ya raia wa nchi hiyo, sio tu kutokana na sababu za ukabila bali pia uongozi mbaya wa kisiasa.
Mwaka 1959, mtawala wa Kitutsi aliyekuwa akiitawala nchi hiyo na kulalamikiwa kuwa utawala wake ulikuwa ukiwaneemesha zaidi Watutsi walio wachache, uliangushwa na Wanyarwanda wa Kabila la Kihutu.
Mabadiliko haya yalifuatiwa na mauaji ya takriban Watutsi
150,000. Walioponea chupuchupu walikimbilia nchi mbalimbali jirani na Rwanda. Ni wakati huu wazazi wa Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame walikimbilia nchi jirani, Uganda yeye akiwa na umri wa miaka miwili.
Baada ya hapo, Wahutu wakaunda Chama cha PARMEHUTU, kikiongozwa na Gregoire Kayibanda, ambaye baadaye alikuwa Rais wa Rwanda.
Mtu angedhani wakati huo kuwa kwa sababu uongozi wa nchi hiyo ulichukuliwa na kudhibitiwa na mtu kutoka kabila la Wahutu waliokuwa asilimia 88 ya Wanyarwanda wakati ule, (Watutsi wakiwa asilimia 11 na asilimia moja Watwa), kusingekuwa na chokochoko tena. Utawala ungekuwa wa amani, wapi?
Mapinduzi ya kijeshi
Kinyume na matarajio, Julai 5, 1973 Serikali hii nayo ilipinduliwa. Mapinduzi haya yalifanywa na jeshi la Wahutu wakiongozwa na Meja Jenerali Juvenal Habyarimana, ambaye naye alikuwa Mhutu.
Cha ajabu, licha ya tofauti hizo za kikabila, mapinduzi hayo yalifanywa na Wahutu walio wengi wakishirikiana na Watutsi wachache. Hii ilitokana na malalamiko kuwa Rais Kayibanda alikuwa akiendesha nchi kama familia yake, akipitisha uamuzi bila kushirikiana na viongozi wengine.
Baada ya mapinduzi hayo, kiongozi huyo mpya alibadilisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusambaratisha chama kilichokuwa kikiongozwa na Kayibanda, PARMEHUTU, badala yake akaunda Chama cha National Revolutionary Movement for Development MRND.
Miaka takriban 17 baadaye kutokana na kile kilichoonekana kama utawala wa kikandamizaji, Watutsi waliokuwa nje ya nchi walishirikiana na Wahutu wa ndani kuanza harakati za kuiangusha Serikali ya Habyarimana.
Harakati hizi ndizo zilizomwingiza madarakani Rais wa sasa, Paul Kagame. Malalamiko kama yale yaliyosababisha mapinduzi dhidi ya mtangulizi wa Habyarimana yakajitokeza tena.
Mtu anayeangalia na kuchambua hali ya mambo ilivyo hivi sasa hachelewi kung’amua kuwa hali kama ile iliyozikumba tawala za tangu utawala wa kifalme wa Watutsi na tawala za Kihutu zinajitokeza tena.
Na hii inaifanya hali iwe tete kuliko wakati wowote. Wengi wanaamini kama yatatokea mapigano au mabadiliko katika Serikali ya Kigali pengine hali inaweza kuwa mbaya kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.
Hivi sasa Wanyarwanda hasa kutoka Kabila la Kitutsi na ambao walikuwa bega kwa bega na Rais Kagame, baadhi ya wasomi na maofisa wa juu kutoka jeshi la RPF wameikimbia Rwanda na tayari kuna kampeni za chini kwa chini kutoka makabila yote mawili kuupinga utawala wa Kagame.
Mbaya zaidi kuna kundi kubwa la vijana waliozaliwa baada ya mauaji ya Rwanda. Hili ni kundi kubwa na mtu yeyote ambaye amekuwa akitembelea kambi za wakimbizi kwa miaka mingi anaelewa ninachoelezea hapa.
Mwaka 1997 nikiwa na waandishi wenzangu tulitembelea kambi za wakimbizi kutoka Rwanda. Kulikuwa na idadi kubwa ya watoto. Mmoja wetu alimuuliza mmoja wa wakimbizi kwa utani “nyinyi mpo kwenye matatizo mbona mnazaa watoto wengi hivi, hamuoni ikiwa mnajiongezea mizigo”?
“Hawa ndio watakuja kuikomboa Rwanda,” alijibu kiongozi wa wakimbizi huku akipigiwa makofi na kundi la vijana waliokuwa pembeni kusikiliza mahojiano, katika kambi ya Mbuba wilayani.
Nadharia hii imekuwa ikiendelea kwa miaka mingi. Hata tulipotembelea kambi nyingine tukiandamana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia wakimbizi Ulimwenguni (UNHCR), Antonio Guateres karibu waandishi wengi hawakuficha hisia zao za kushangazwa na kasi ya kuzaana katika kambi za wakimbizi.
Fikiria kwa utaratibu huu watoto waliozaliwa tangu mwaka 1994 ni watu wazima. Kama ni wanajeshi ni jeshi kubwa tena lenye hamasa kubwa ya kurudi katika nchi yao Rwanda katika wakati ambapo wanaona kikwazo ni Kagame na Serikali yake.
Hivi Kagame anajua kuwa kundi hili halibanwi na tuhuma za mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994? Hata wale wanaotafutwa sio tena kitisho dhidi ya Serikali ya Kigali sababu ni wazee sasa, wa kuogopa ni jeshi hili kubwa la vijana.
Hawa Kagame anawabana na sheria gani? Isipokuwa kwamba wanajiandaa kupigana na Serikali yake kama yeye alivyofanya kuipindua Serikali ya Habyarimana akitokea Uganda?
Kibaya zaidi ni kuwa makundi haya katika ukanda wa Maziwa Makuu, wana mawasiliano na kwa nyakati fulani yanasaidiana.
CHANZO: kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni
No comments:
Post a Comment