Agathe Uwilingiyimana:Waziri mkuu pekee mwanamke
Rwanda
ALIKUWA waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Rwanda. Hadi sasa hajatokea mwanamke mwingine kushika nafasi hiyo nchini humo.
Ni Agathe Uwilingiyimana aliyeshika wadhifa huo kwa miezi ipatayo kumi tu -- tangu Julai 18, 1993 hadi Aprili 6, 1994 alipouawa mwanzoni mwa mauaji ya halaiki yaliyotokea nchini humo.
Mama huyo ambaye alikuwa ni Mhutu, alizaliwa Mei 23, 1953 huko Nyaruhengeri, katika nchi ambayo wakati huo ilikuwa inaitwa Rwanda-Urundi. Wakati huo nchi hizo ambazo leo ni mbili zilikuwa nchi moja zikitumia jina hilo.
Akingali mdogo, familia yake ikahamia Kongo-Kinshasa ambako baba yake alikuwa anafanya kazi. Walirejea Rwanda wakati Agathe akiwa na umri wa miaka minne.
Agathe alisoma vyema na kujikita katika masuala ya huduma kwa umma akiwa na umri wa miaka 20 tu. Mwaka 1976, alihitimu kidato cha sita na kufaulu vyema hisabati na kemia, akawa mwalimu kabla ya kuolewa na Ignace Barahira mwaka huo ambapo walipata mtoto wao wa kwanza na baadaye kupata watoto watano.
Akiwa na miaka 30 (mwaka 1983) akafundisha kemia kwenye Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda na baadaye alipata Shahada ya Sayansi (B.Sc) mwaka 1985.
Mwaka 1986 akaanzisha harakati za vyama vya ushirika vya kukopeshana, jambo ambalo lilivutia nadhari ya serikali na hatimaye mwaka 1989 akawa Mkurugenzi katika Wizara ya Afya.
Mwaka 1992 akajiunga na chama cha upinzani cha Republican and Democratic Movement (MDR) ambapo miezi minne baadaye akateuliwa na Dismas Nsengiyaremye (aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza kutoka upinzani) kuwa Waziri wa Elimu chini ya serikali ya Rais Juvenal Habyarimana iliyoamua kugawana madaraka na vyama vingine vitano vya upinzani.
Julai 17, 1993, baada ya mkutano baina ya Habyarimana na vyama vyote vitano, Agathe Uwilingiyimana (yaani Mtu Anayemtegemea Mungu, tafsiri yake kwa Kiswahili) akawa mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu wa Rwanda, akichukua nafasi ya Dk. Nsengiyaremye, aliyekuwa amemteua kuwa Waziri wa Elimu.
Hata hivyo, Nsengiyaremye
hakupendezewa na Agathe kuwa waziri mkuu, vilevile wapinzani wenzake walikuwa hawampendi wakifikiri alikuwa kibaraka wa Habyarimana. Hivyo, siku ya kuteuliwa kwake kuwa waziri mkuu, Nsengiyaremye, alimsimamisha Agathe uanachama wake katika MDR akidai ilikuwa si vyema Agathe kutokishirikisha chama cha waasi wa Kitusi cha RPF katika serikali yake.
Mgogoro huo ulisababisha Habyarimana kumwachisha kazi Agathe siku 18 tu baada ya kumteua. Hata hivyo, mama huyo aliendelea kukaimu wadhifa huo kabla ya kuundwa kwa serikali mpya. Nafasi yake ikawa imepangwa kuchukuliwa na Faustin Twagiramungu.
Hata hivyo, Agathe aliuawa miezi minane baadaye, Aprili 1994, akiwa bado katika wadhifa huo, baada ya kuahirishwa kuapishwa kwa serikali yenye kujumuisha vyama vingi zaidi kulikokuwa kufanyike Machi 25, 1994. Hii ilitokana na RPF kutofika kwenye hafla hiyo.
Mazungumzo kati ya Habyarimana na RPF hayakufanyika kwani ndege ya rais huyo iliyokuwa inatoka Dar es Salaam, Tanzania, ilipigwa makombora wakati ikitua uwanjani Kigali, saa 2:30 usiku, Aprili 6, 1994, ambapo rais huyo na watu wengine walikufa.
Uwilingiyimana na mumewe waliuawa kesho yake, Aprili 7, 1994, na majeshi ya Watusi. Watoto wao walipona wakakimbilia Switzerland. Agathe akafariki akiwa na umri wa miaka 40.
Ni Agathe Uwilingiyimana, mama wa Kihutu aliyekuwa na taswira yenye mvuto wa Kihutu. Hadi anakufa alikuwa bado waziri mkuu wa Rwanda na mwanamke wa kwanza katika nchi hiyo kushika wadhifa huo. Hajatokea tena mwanamke mwingine!
CHANZO: Walusanga Ndaki
No comments:
Post a Comment