Wednesday, February 12, 2014

BURIANI LT GEN SP MAYUNGA



Buriani Luteni Jenerali Mayunga

KATI ya viongozi ambao nilipenda kusikia kauli zao kuhusu Luteni Jenerali Silas Mayunga, aliyefariki wiki iliyopita, Agosti 5, nchini India, ni Waziri wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali (mstaafu) Abdulrahman Kinana.
Kwa nini Kinana? Kwa sababu anajua masuala ya jeshi katika sura mbili. Kwanza kama mwanajeshi; pili Waziri wa Ulinzi. Lakini kubwa zaidi, anafahamiana kwa karibu na Mayunga.
Itakumbukwa Novemba mosi, 1978, majeshi ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin yalivamia Mkoa wa Kagera. Uvamizi huo ulimsukuma Mwalimu Nyerere kuashiria ushindi kabla vita kuanza.
Nyerere aliashiria ushindi kabla vita kuanza akisema; “sababu ya kumpiga tunayo, nia ya kumpiga tunayo na uwezo wa kumpiga tunao.” Hakika, kauli hii ilihitaji si tu risasi za kutosha, mizinga au makombora na silaha za kila aina kuisimamia, bali mashujaa wa mstari wa mbele vitani.
Ilikuwa kazi kubwa, na kwa kweli ilikuwa ni juu ya makamanda wa mstari wa mbele kuamua kuivunjia hadhi kauli hiyo ya Amiri Jeshi Mkuu au kuisimamia kufa au kupona ili ibaki kuwa ya ukweli.
Hivyo basi, ni kauli au hotuba iliyopaswa kutetewa, kupiganiwa kufa au kupona ili kuuthibitishia ulimwengu; Amiri Jeshi Mkuu -Rais Nyerere alikuwa sahihi kutangaza uwezo, nia na sababu za kumpiga Amin upo.
Ingawa makamanda wa mstari wa mbele walikuwa na zana za kivita, lakini hotuba ya Mwalimu iliwaongezea silaha ya ziada ambayo ni uzalendo.
Miongoni mwa wapiganaji waliotwikwa dhima hiyo nzito ni pamoja na Luteni Jenerali Silas Mayunga, sambamba na wapiganaji wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Watanzania kwa ujumla, waliotoa ng’ombe hata kuku kulisha wapiganaji uwanja wa mapambano.
Mstari wa mbele katika uwanja wa vita, Luteni Jenerali Silas Mayunga na wenzake, kazi ilikuwa moja tu-kufa au kupona ili kulinda si tu hadhi ya Tanzania, heshima ya wapenda haki duniani.
Ni vita hii ya Kagera ndiyo inayotajwa kumtambulisha zaidi Luteni Jenerali Mayunga ndani ya JWTZ na Jeshi la Uganda. Vita hiyo ilimpambanua ni mpiganaji wa aina gani akiwa mstari wa mbele.
Luteni Jenerali Mayunga ni nani?
Kama ilivyo kwa watu wengi mashuhuri dunia, haikuwa rahisi kumtabiria mtoto mdogo aliyezaliwa Maswa, Shinyanga, mwaka 1940; eti siku moja ataipigania nchi yake kufa au kupona, akiwa katika uwanja wa mapambano ya risasi, mizinga na makombora mazito.
Bila shaka, hata alipokuwa shuleni Bwiru Sekondari, Mwanza, walimu na wanafunzi wenzake hawakujua unyeti wa Silas Mayunga nchini, miaka kadhaa iliyofuatia.
Pengine hata naye hakujua uzito wa uamuzi wake wa kuanza maisha mapya ya kijeshi alipojiunga, na kwa mara ya kwanza na Jeshi la kikoloni, (Tanganyika Rifles) Januari 10, mwaka 1963.
Safari yake kijeshi imegusa nchi za Israel na Canada, akihitimu mafunzo ya kijeshi Julai 26, mwaka 1963 nchini Israeli na miaka 10 baadaye (1973), akafuzu kozi ya unadhimu na ukamanda wa jeshi nchini Canada. Kozi ya Ukamanda wa Juu wa Jeshi alihitimu mwaka 1974 nchini.
Juni 21, mwaka 1995, ni siku ambayo Mayunga alijiwekea rekodi binafsi ya kushika cheo cha juu jeshini, akipandishwa cheo kuwa Luteni Jenerali na miezi sita baadaye (Desemba 31, 1995) alistaafu.
Mti mkavu akiwa jeshini
Mayunga ni kamanda kiongozi. Amekuwa Mkurugenzi wa Mafunzo makao makuu ya jeshi, Kamanda wa Brigedi ya 202 ya Tabora, na Kamanda wa Divisheni za 20 na 30 za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Huwezi kuzungumzia Operesheni Chakaza wakati wa vita dhidi ya majeshi ya Idi Amin bila kumtaja kiongozi wa operesheni hiyo ambaye ni Luteni Jenerali Mayunga.
Katika Operesheni Chakaza, Mayunga ndiye aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya 206. Ndani ya Jeshi la Uganda Mayunga ana historia muhimu. Amekuwa Kamanda wa Kikosi Maalumu cha JWTZ nchini Uganda kati ya 1979 na 1980.
Lakini ukiondoa pilikapilika za kijeshi, Mayunga amekuwa Mkuu wa Mkoa Singida mwaka 1977 – 1978, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria mwaka 1989 hadi 1998 na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) 1998 na 2002, alipostaafu.
Kinana na Mayunga Liberia
Kama nilivyoeleza awali, nimezungumza na Kinana. Amekumbuka mengi kuanzia pilikapilika za kivita za Mayunga akiongoza sekta ya Mbarara, sambamba na jukumu zito la kufundisha majeshi ya Uganda ili si tu kusafisha masalia ya Idi Amin; bali kuliweka upya jeshi la Uganda.
“Wakati ule (vita ya Kagera) kulikuwa na sekta mbili. Sekta ya Masaka ikiongozwa na Musuguri na sekta ya Mbarara akiongoza Mayunga,”
“Anazo sifa nyingi muhimu kama kiongozi. Kwanza, uwezo wa kujichanganya na watu wote. Wanajeshi wote walimpenda kama kiongozi, akiwa anaongoza vikosi vyote sekta ya Mbarara na makao yao makuu yakiwa mji wa Mbarara -Uganda, hapo alikuwa akifundisha majeshi ya Uganda.
“Nakumbuka pia mwaka 1994, nikiwa Waziri wa Ulinzi naye akiwa Balozi wetu katika nchi zote za Afrika Magharibi, Umoja wa Mataifa ulituomba kupeleka wanajeshi wa kulinda amani Liberia.
“Tulipeleka wanajeshi 1,000, nikiwa na Mayunga tuliwatembelea wanajeshi wetu kwa kweli aliwapa hotuba nzuri sana ya kuhimiza uzalendo, wanajeshi wetu walifurahi kumwona na kuzungumza na Mayunga wakitambua sifa yake ndani ya jeshi, akiwa vitani Uganda,”
“Tulikuwa pale siku tano, lakini kikubwa zaidi niligundua kuwa aliweza kuwa karibu sana na watu wa hizo nchi alizokuwa akiiwakilisha Tanzania na hiyo ndiyo sifa yake kuu. Ni mtu wa kuchanganyika na watu wote,” anaeleza Kinana.
Mayunga
Nimebahatika kuzungumza na baadhi ya wapiganaji walioshiriki vita ya Kagera. Kwao, Mayunga ni mti mkavu usiochimbwa dawa. Kwa mujibu wa simulizi zao, Mayunga alikuwa akiwajaza uzalendo, ujasiri na kuwaondolea uchovu kila walipokuwa wakisonga mbele kumkabili adui.
Kwa maelezo yao, Mayunga ni mpiganaji aliyedhihirisha kuwa ushindi wa kivita hautokani na kigezo cha silaha bora pekee, bali ni wapiganaji jasiri, wazalendo na hodari katika kupiga hatua kusonga mbele na si hatua za kurudi nyuma-kumkimbia adui.
Huyo ndiye Mayunga ambaye hakufa akiwa uwanja wa mapambano akihangaika kuikomboa nchi yake dhidi ya adui. Ndiyo, hakufa kwa risasi, mizinga wala makombora ya adui vitani.
Pamoja naye, tunawaenzi makamanda wetu waliofia vitani na waliorudi hai, walimsogeza adui nyuma na kuyapa ushindi majeshi ya Tanzania na Watanzania.
Wapiganaji wote kuanzia vikosi vya nchi kavu, maji, anga na intelijensia ya kijeshi (military intelligence) katika JWTZ na nchi kwa ujumla, hatuna budi kusema; ingawa tumepoteza kamanda mwingine aliyesonga mbele mstari wa mbele vitani, mwaka 1978 lakini tunaridhika ametimiza wajibu wake kwetu, raia wenzake.
Ameishi kwa kutii mamlaka ya nchi. Ameishi kwa kutii raia wenzake, ameishi kwa mujibu wa tamaduni za Kitanzania. Huyu si kamanda wa kijeshi pekee, bali ni mpigania haki duniani.
Ingwa tunamlilia lakini tunaridhika, tunashukuru na kujipongeza kwa kugonganisha ‘glass’ tukisema imewezekana, ametimiza wajibu.
Ewe Luteni Jenerali Mayunga, hakufa kwa risasi, mizinga wala milipuko yoyote pengine kama familia yako ilivyohofia ukiwa vitani lakini sasa umekufa ukiwa kitandani ukitibiwa. Buriani Kamanda Mayunga. Tunasikitika kwa kifo, lakini tunafurahi umetimiza wajibu.
CHANZO:http://www.raiamwema.co.tz/

No comments:

Post a Comment