Tuesday, February 11, 2014

HOSNI MUBARAK: MCHEZA SKWASHI ALIYEEPA MISHALE MINGI



Mara kadhaa, Mubarak aliapa kuendelea kuitumikia Misri hadi pumzi yake ya mwisho. Hotuba ya Februari 1,  alisema: “Taifa langu kipenzi... ndiko ninakoishi, nimeipigania, nimeilinda ardhi yake, utu wake na masilahi. Kwenye ardhi yake, nitafia. Historia  itanihukumu kama ilivyofanya kwa wengine.” 
·         Mubarak pia alinusurika mara sita kuuawa, ingawa  jaribio linalokumbukwa zaidi ni lile la mwaka 1995, Addis Ababa,  Ethiopia  alipokwenda kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika (AU)

Cairo. Kama wasemavyo wahenga, ukimwona nyani mzee ujue kaepa mishale mingi, ndivyo ilivyo kwa Hosni Mubarak, mwanasiasa  mkongwe ambaye ameachiwa huru na mahakama moja ya Misri wiki iliyopita.
Mubarak, amekoswa na risasi mara kadhaa, karibuni amechomoka kwenye hukumu ya kifo iliyokuwa ikimnyemelea kutoka kwa wabaya wake, Muslim Brotherhood tangu walipomwangusha mwaka 2011.
Ndiyo maana, bado likitajwa jina lake, bila shaka wengi wanamfahamu, kumkumbuka kama Rais wa Misri, kiongozi aliyeiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 30 hadi alipoondolewa madarakani kwa nguvu ya harakati.
Kabla ya kuingia madarakani, Mubarak alikuwa mtu asiyejulikana hata Misri ambako alikuwa makamu wa rais wa Anwar Sadat ambaye aliuawa kwa risasi mwaka 1981.
Pia, haikuwa rahisi kudhani kuwa Mubarak angedumu madarakani kwa muda mrefu kiasi hicho.
Kifo cha ghafla cha Sadat ambaye aliuawa na wanaharakati wa Kiislamu kwenye gwaride la kijeshi mjini Cairo kikambeba Mubarak,  ambaye naye alinusurika kifo kwenye shambulizi hilo.
Tangu wakati ule, Mubarak pia alinusurika mara sita kuuawa, ingawa  jaribio linalokumbukwa zaidi ni lile la mwaka 1995, Addis Ababa,  Ethiopia  alipokwenda kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika (AU) baada ya gari lake la kifahari kushambuliwa.
Kamanda huyo wa zamani wa Jeshi la Anga la Misri pia aliweza kubakia madarakani kwa kujiweka karibu na wakubwa, hasa wa nchi za Magharibi ikiwamo Marekani, akikandamiza apendavyo upinzani nchini mwake.
Ghafla, miaka michache iliyopita upinzani nchini humo ulibadili mbinu ukamwandama, akakosa kuungwa mkono na nchi za Kiarabu ambazo pia baadhi yake zilikuwa katika mizozo.
Harakati hizo zilimfanya aamue Februari Mosi kutangaza kutokugombea tena urais baadaye mwaka huo, tangazo  lilifuatia  machafuko makubwa jijini Cairo na katika miji mingine.
Harakati hizo ziliendelea hadi Februari  10 pale alipotangaza kupitia televisheni kwamba alikuwa tayari kukabidhi madaraka kwa makamu wake, ingawa yeye akibakia rais.
Kesho yake, makamu wake, Omar Suleiman  alitangaza kuwa bosi wake alikuwa ameamua kujiuzulu na baraza kuu la kijeshi lingekuwa na jukumu la kuiongoza nchi.
Kusimama kizimbani
Ilipofika Mei 24, 2011, maofisa wa mahakama  walitangaza  kwamba Mubarak, pamoja na wanawe, Alaa na Gamal wangesimama kizimbani kwa tuhuma za kuhusika na vifo vya wapinzani wa Serikali wakati wa maandamano.
Ndipo Juni  2, 2012  Mubarak alitiwa hatiani kwenye tuhuma ngumu za mauaji ya waandamanaji walioshiriki harakati za kumwondoa madarakani zilizoanza Januari 25 , 2011.  Yeye (Mubarak) pamoja  na Waziri wa Mambo ya Ndani, Habib Al-Adly, walitupwa jela maisha kwa makosa yaliyokuwa yakiwakabili.
Januari 2013, Mahakama Kuu ya Misri iliruhusu rufaa dhidi ya hukumu ya Mubarak na  al-Adly na kuamuru kesi isikilizwe upya. Mubarak na wanawe walikuwa wakisubiri kupandishwa kizimbani kwa madai ya rushwa ambayo walikuwa awali wamefutiwa.
Hata hivyo, Agosti 19, Mubarak aliachiwa na kufutiwa madai ya rushwa na ubadhirifu ya fedha za umma, jambo ambalo lilitoa nafasi kwa wakili wake kudai kuwa hakukuwa na sababu za kuendelea kumweka kizuizini.
Maofisa wa mahakama waliliambia Shirika la habari la The Associated Press kwamba Mubarak angeachiwa huru kwa  kuwa alikuwa tayari amekaaa jela kwa muda wa kutosha kabla ya kesi yake kusikilizwa, kama inavyotakiwa kisheria. 
Mbali ya kuachiwa huru, lakini Mubarak ameshtakiwa Jumapili kwa kosa lingine la rushwa linalohusu kupokea zawadi akiwa madarakani. Kwa sasa yuko kifungoni nyumbani kwake.
Maisha yake binafsi
Mubarak alizaliwa  mwaka 1928  kwenye kijiji kidogo katika Jimbo la Menofya karibu na Cairo. Kwa muda mrefu, alikuwa kiongozi ambaye alipenda maisha yake yasijulikane kwa wengi.
Alifahamika zaidi kama, Muhammad Hosni Sayyid Mubarak, kiongozi ambaye aliapishwa Oktoba 14, 1981, siku nane baada ya kuuawa kwa Anwar  Sadat.
Alimuoa  Suzanne mwaka 1959 ambaye ni Mwingereza na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Marekani mjini Cairo, ambaye walizaa naye watoto wawili, Gamal na Alaa.
Binafsi, Mubarak hakuwahi kuvuta sigara au kunywa pombe, akiwa mtu  wa mazoezi yaliyoweka vizuri siha yake.
Akiwa bado mdogo, marafiki zake wanaeleza kuwa alilalamikia maisha ya urais, utaratibu wa kuishi Ikulu, ingawa yeye alianza siku kwa mazoezi gym au kucheza skwashi.
Licha ya kutokufahamika kimataifa, lakini alitumia jeuri ya ukakamavu wa kijeshi kufanya mambo mengi yakiwamo ya kunyamazishwa wapinzani wake, kuzima madai ya kupanga kuuawa kwa Sadat, kuingia mkataba wa amani na Israel na kujijengea sifa binafsi.  
Mfumo wa utawala wake
Mara kadhaa, Mubarak aliapa kuendelea kuitumikia Misri hadi pumzi yake ya mwisho. Hotuba ya Februari 1,  alisema: “Taifa langu kipenzi... ndiko ninakoishi, nimeipigania, nimeilinda ardhi yake, utu wake na masilahi. Kwenye ardhi yake, nitafia. Historia  itanihukumu kama ilivyofanya kwa wengine.”
Kwa ufupi, Hosni Mubarak aliitawala Misri kama nchi ya kidemokrasia iliyojengwa kwa misingi ya kijeshi.
Kwa miaka 30 ya utawala wake, Misri ilikuwa kwenye hali ya hatari, dharura, akitoa madaraka kwa wasaidizi wake kukamata wapinzani na kuingilia uhuru wao.
Serikali yake ilitetea guvu zilizotumika kuwazima wapinzani wake wakiwamo wanaharakati wa Kiislamu, wakiwamo magaidi ambao waliilenga Misri kwa muda wote wa utawala wake, wakipiga vivutio vya kitalii.
Kwa muda mrefu alifaulu kuipa nguvu Misri kiuchumi na kupata maendeleo ambayo yalimaanisha kukubalika kwake machoni mwa Wamisri.
Watu wa karibu na Mubarak walisema kuwa afya yake, uwezo na umri vilimpiga chenga, ingawa mara kadhaa wasiwasi kuhusu afya yake ulizuka na kupita.
Uvumi kuhusu afya yake ulishika kasi aliposafiri kwenda Ujerumani, Machi 2010  kufanyiwa upasuaji wa kibofu cha mkojo. Hofu ilizidi alipokosekana hadharani na kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, hofu hiyo ilizimwa na maofisa wa Serikali yake ambao walisambaza habari kwenye vyombo vya habari vya Kiarabu na Israel. Gamal Mubarak kama mrithi
Siku za machafuko ya kisiasa kwenye miji mbalimbali ya nchi zilimlazimisha Mubarak hatimaye kutangaza makamu wake, yaani Gamal, mwanawe.
Januari  29,  mkuu wa ukachero, Omar Suleiman  alipandishwa cheo na kuwa makamu wake, hizo zikiwa mbinu za Mubarak  kusaka kuungwa mkono na jeshi.
Hadi wakati ule hakukuwa na mrithi wake, ila wasiwasi ulikuwa kwa Gamal, kijana wa miaka 40 na mwekezaji kwenye masuala ya  benki kwamba ndiye aliyekuwa akiandaliwa kwa kazi hiyo ya urithi.
Gamal, kwa upande wake alisisitiza kutokuwa na nia ya urais, ingawa alikuwa akikua na kuongezeka kwenye uongozi wa NDP, mmoja wa wapigania mabadiliko.
Wataalamu wa historia wamekuwa wakieleza kuwa tangu mapinduzi ya mwaka 1952, isingekuwa ajabu kwa Gamal kumrithi  baba yake akiwa Rais, ingawa angekuwa na wakati mgumu kukubalika.

No comments:

Post a Comment