Ni ndege ambayo kila mmoja angependa
kuiona, kuipanda
Hakuna shaka yoyote kuwa Rais wa
Marekani akisafiri kokote duniani akitumia ndege ya kijeshi, basi hupewa jina
la ‘Air Force One’. Ukweli si ndege maalumu yenye jina hilo, lakini ndege inayopewa
jina hili ni alama ya ndege ya rais wa nchi hiyo.
Jina hilo hutumika kwa ndege mbili kubwa aina ya Boeing
747-200B zenye namba 28000 na 29000, zinazotumiwa na rais akiwa safarini
ndani na nje ya Marekani na moja anayosafiria ndiyo huitwa kwa jina hilo.
Ndege zote hizo husimamiwa na Jeshi la Anga la nchi hiyo.
Kwa jeshi la nchi hiyo ishara kwa ndege hizo ni VC-25A.
Air Force One ni moja ya ishara maarufu kwa urais wa Marekani na
si kwa Marekani pekee, bali imekuwa kwa ulimwengu mzima. Ndege zote
zimeandikwa maandishi makubwa “United States of America,” bendera ya nchi
hiyo na nembo ya rais wa nchi hiyo.
Ndege hii tofauti na za kawaida zilizozoeleka, inao uwezo wa
kujazwa mafuta ikiwa angani kwani haina kiwango ama urefu maalumu wa kusafiri inaweza
kumfikisha rais huyo popote duniani kwa usalama wa hali ya juu.
Ndani ya ndege vifaa vya umeme vimetengenezwa kwa ugumu ambao
haviwezi kusababisha hitilafu ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya abiria. Ina
vifaa vizito vya mawasiliano vyenye teknolojia ya hali ya juu inayowezesha
kufanya kazi kama sehemu ya kamandi ya kijeshi (CP) ikiwa angani kama kuna
shambulio nchini mwao.
Ndani yake rais na abiria wengine wanafaidi nafasi kubwa ambayo
ni kama futi 4,000 za mraba zilizo katika ghorofa tatu ikiwa ni pamoja na
sehemu kubwa kwa ajili ya Rais, yenye chumba cha kifahari cha kulala, ofisi,
choo, chumba cha mikutano.
Pia, kuna sehemu ya matibabu ambayo ina chumba cha upasuaji na
daktari angalau mmoja anatakiwa kuwa ndani wakati ndege hiyo ikiwa safarini,
pamoja na wahudumu wengine wa afya. Kuna sehemu mbili za jiko ambazo zinaweza
kutumika kuandaa chakula cha watu 100 kwa wakati mmoja.
Air Force One pia ina sehemu kwa ajili ya wasaidizi walinzi na
watu wengine wanaoongozana na rais safarini ikiwamo waandishi wa habari ama
wageni wengine. Kuna ndege kadhaa za mizigo ambazo zinaongozana na ndege
hiyo zikiwamo za kuongeza mafuta ili kuweza kumuhudumia Rais iwapo atakuwa
angani kwa muda mrefu.
Air Force One inahudumiwa na Kikosi cha Safari za Rais ikiwa ni
sehemu ya maofisa usalama wa Ikulu ya Marekani kilichoanzishwa mwaka 1944 chini
ya Rais Franklin D. Roosevelt.
No comments:
Post a Comment