SIMON Bolivar alikuwa
mwanamapinduzi wa Venezuela aliyeiaga dunia Desemba 17, mwaka 1830 akiwa na
umri wa miaka 47. Kuna wanaoamini kwamba alikufa kwa kulishwa sumu. Miongoni
mwao ni Hugo Chávez, Rais wa Venezuela, ambaye kwa sasa amefariki baada ya kutibiwa Cuba kwa ugonjwa wa saratani.
Oktoba 7, mwaka huu,
Chávez kwa mara ya nne alishinda uchaguzi wa urais. Alishinda licha ya ule
msaada wa dola zisizopungua milioni 50 ambazo inasemekana Marekani mwaka huu
iliwapa wapinzani wake wamshinde.
Lakini yeye ndiye
aliyewatwanga na katika uchaguzi wa magavana uliofanywa Jumapili iliyopita
chama chake cha Kisoshalisti kiliongeza idadi ya viti vya magavana
ilivyoshinda.
Januari, kama angekuwa
mzima, Chávez angeapishwa kwa muhula mwingine wa urais wa miaka sita.Chávez
anaona fahari kujinasibisha kuwa ni mrithi wa dhati wa Bolivar.Tangu ashike
madaraka miaka 13 iliyopita hachoki kukumbusha kwamba siasa zake za ‘Chavismo’
zinalenga kuyatekeleza mapinduzi ya kibolivar.
Vyombo vya habari vya
Marekani na vya vibaraka wake vimezoea kumfanyia tashtishi na kumcheza shere
Chávez vikimfananisha na bahaluli au Juha Kalulu.Hayo si ya ajabu kwani ni
kawaida yao kumkebehi kila kiongozi wa wanyonge anayethubutu kusimama kidete na
kwenda kinyume cha ubepari wa utandawazi.
Kwa hakika, Chávez
alianza kufanyiwa vitimbwi alipotangaza mara ya mwanzo kwamba atawania urais
1998. Alisema anataka kuijenga upya nchi yake kwa misingi mipya. Wengi
walimcheka.
Kwa mtizamo wao katika
mwanzo wa karne ya 21 Chávez alikuwa mtu mwenye fikra za kizamani zilizopitwa
na wakati. Alikuwa mwanamapinduzi wa mrengo wa kushoto aliyekuwa akiungwa mkono
na Wakomunisti wachache waliobaki nchini mwake na makundi kama sita ya mielekeo
mbalimbali ya kisoshalisti.
Nadhani Tanzania hii leo
akisimama mtu na kusema anataka kuurejesha ujamaa ataonekana mwehu — hata
akisema kama ujamaa anaoutaka ni wa aina mpya. Itakuwa hivyo kwa sababu wengi
wetu tuna fikra finyu na tumezoea kuyumbishwa na wimbi litokalo nchi za
kimagharibi.
Cháveza na mbwembwe za
aina yake.Pia ana mtindo wa aina yake wa uongozi ulio na dosari zake lakini wenye
kumpa haiba kubwa. Si watu wote wenye kumpenda. Maadui zake wanasema ulimi wake
hauna akili. Hauna ubongo.
La muhimu ni kwamba yeye
ni miongoni mwa viongozi wachache wa dunia hii wenye kuwajali watu wao. Ni
kiongozi ambaye Bara la Afrika halikujaaliwa kumpata. Inasemekana kwamba nchi
yake ni ya tano, ikiwa pamoja na Finland, yenye wakaazi wenye furaha mno
duniani. Hayo si mafanikio madogo.
.jpg)
Ufukara wakutupwa
umepungua kutoka asilimia 40 katika 1996 na kufikia sasa kasoro ya asilimia
saba. Mwaka 1990 asilimia 7.7 ya watoto walikuwa wakifa kutoka na utapiamlo
lakini sasa takwimu hiyo imeshuka na kuwa asilimia 2.9.
Tangu Chávez awe rais
idadi ya wasio na ajira imepungua kutoka asilimia 11.3 na kuwa asilimia 7.7.
Katika kipindi cha miaka 10 uchumi wa Venezuela umetanuka kwa asilimia 47.7 na
leo uchumi huo ni madhubuti kushinda uchumi wa Marekani na nchi kadhaa za
Ulaya.
Kuna mafanikio mengine
ambayo Venezuela imeyapata ikiongozwa na Chávez. Wazee zaidi ya milioni mbili
na laki moja wanalipwa malipo ya uzeeni na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Kabla
ya Chavez watu 387,000 tu ndio waliokuwa wakilipwa malipo hayo.
Elimu ni bure kutoka ya
chekechea hadi ya chuo kikuu. Wananchi milioni tano wanalishwa bure na
serikali. Venezuela haina watoto masikini wa mitaani au chokora kama
wanavyoitwa Kenya. Dawa zinapatikana kwa bei rahisi. Venezuela pia ina maduka
mahsusi yenye kuwauzia watu wa chini vyakula na vitu vingine kwa bei za chini.
Swali la kujiuliza ni:
Ilikuwaje Venezuela chini ya Chávez ikaweza kupiga hatua kubwa hivyo katika
muda mfupi?

Alipoingia Ikulu mara ya
kwanza 1998, Chávez aliingia akiwa na kikapu cha ahadi akilini mwake. Aliahidi
kwamba ataufyeka ufisadi uliokuwa ukiila nchi yake kama unavyozila nchi nyingi za Afrika.
Aliahidi kwamba atakuwa
na sera mbadala kwa nchi yake, sera ambayo itajitenga kabisa na ile ya uchumi
wa kiliberali mamboleo iliyokuwa ikifuatwa nchini humo na ambayo sisi Tanzania
na kwingineko Afrika tumeing’ang’ania.
Badala ya kutegemea zile
ziitwazo ‘nguvu za soko’ na utandawazi serikali yake ikaanza kupanga maendeleo
ya nchi kwa kutumia rasilimali zake na sio kwa kuwategemea wawekezaji.
Kadhalika, Chávez alizivunja nguvu Shirika la Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF)
na Benki Kuu ya Dunia katika uendeshaji wa uchumi wa nchi yake.
Alichofanya ni
kuthibitisha kwamba kuna sera mbadala za kiuchumi zinazoweza kufuatwa na nchi
kama zetu badala ya hizi tunazozikumbatia.
Jengine alilolifanya
Chávez ni kuwa macho na kutoipa Marekani nafasi ya kuichezea nchi yake kinyume
cha wafanyavyo viongozi wetu. Kwa mfano, amekataa kuziruhusu ndege za Marekani
kuingia katika anga ya Venezuela kwa kisingizio cha kuwafukuzia wenye kufanya
biashara haramu ya mihadarati. Viongozi wetu wanaipa Marekani fursa hiyo kwa
kisingizio cha kuwafukuzia magaidi.
CHANZO: http://www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment