Burundi
na miaka 16 ya kuuawa Ndadaye
Na William Kapawaga - Imechapwa 01 November 2009
MIAKA 16 imepita tangu Burundi itikisike kutokana na kuuawa kwa
aliyekuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye. Tukio
hilo lilitokea mwaka 1993.
Chimbuko lake ni Jeshi la Burundi kuasi na kusababisha mauaji ya
kinyama kwa wananchi wasio na hatia yoyote.
Hali ya mambo bado haijatengemaa sawasawa katika nchi hii, pamoja na
kuwepo na utawala wa kiraia ulio chini ya Rais Pierre Nkurunzinza. Kuna mauaji
ya chini kwa chini na hali ya kutokuaminiana miongoni mwa wanasiasa.
Ndadaye aliyezaliwa 28 Machi, 1953 katika Mkoa wa Muramvya, ni msomi
aliyepata elimu ya msingi kwenye mji wa Mbogora, mkoani Gitega mwaka 1960 hadi
1966.
Aliendelea na masomo ya juu na baadaye kuwa mwalimu na mtumishi wa
benki.
Baada ya kushamiri kwa vita vya kikabila huku raia wengi wa kabila
lake la Wahutu na Watutsi wachache, wakiuliwa kinyama na serikali ya kijeshi ya
Burundi, kupitia kwa marais tofauti, Michael Micombero, Jean Babtist Bagaza na
Pierre Buyoya, Ndadaye aliamua kuanzisha kundi la msituni ili kuleta mapinduzi,
akilenga kusaidia kulinda haki za Wahutu.
Kuongezeka kwa makundi ya waasi wa Kihutu porini, yaliyokuwa
yakipambana na serikali ya Buyoya, kulichagiza pande zinazohusika kukaa pamoja
ili kutafuta muafaka na shinikizo la jumuiya ya kimataifa na nchi za Maziwa
Makuu.
Shinikizo hizo zilifanikisha pande hizo hasimu kukaa pamoja kwa
mazungumzo yaliyofanyika Arusha na Dar es Salaam, chini ya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, na hatimaye mwaka 1992 katiba mpya iliundwa ili kuandaliwa
uchaguzi wa kidemokrasia mwaka uliofuata.
Uchaguzi huo wa 1993 ndio uliomwingiza madarakani Ndandaye baada ya
kumbwaga Buyoya aliyekuwa ofisa mkubwa wa jeshi la Burundi.
Siku chache baada ya ushindi wa Ndadaye, kupitia chama chake cha
FRODEBU, hatimaye 10 Julai, 1993, aliapishwa na kuwa rais wa kwanza wa
kuchaguliwa huku akimteua Alphonce Kadege kutoka chama cha upinzani cha UPRONA,
kuwa makamu wake wa rais.
Kuwashirikisha wapinzani katika serikali kulileta matumaini makubwa
kwa wananchi wa Burundi, huku kwa muda wa miezi mitatu mabadiliko makubwa ya
miundombinu na huduma za kijamii yakianza kuonekana kutokana na kufuta sera za
kikabila.
Lakini kama ilivyo kwa msemo wa Waswahili kuwa “kizuri hakidumu,”
ghafla ndoto ya Warundi ya kuingia katika utawala bora, ilizimika.
Ulikuwa ni usiku wa mshtuko kwao, kwa Afrika na dunia nzima pale
redio ya taifa ilipotangaza asubuhi kuwa rais Ndadaye ameuawa na askari wa
Kitutsi walioamua kuasi katika makazi yake jijini Bujumbura.
Mauaji yake yaliibua wimbi la mauaji ya kinyama dhidi ya Wahutu na
wanajeshi wa serikali kutajwa kuhusika hadi kuthubutu kuipindua serikali ya
kiraia katika mapinduzi yaliyofanikishwa na Meja Buyoya kwa mara nyingine.
Inakadiriwa raia 300,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Wahutu,
waliuawa huku maelfu ya wengine wakigeuka wakimbizi na kukimbilia nchi za
jirani.
Takwimu za mwaka 2005 zinaonyesha kuwa nchi hiyo ina wananchi
wapatao milioni saba.
Makabila makubwa yanayojulikana nchini Burundi ni Wahutu wanaochukua
asilimia 90 ya wananchi wote, wakati asilimia 9 ni Watutsi na waliobaki ni
kabila dogo la Watwa.
Kiasili, Warundi ni wakulima wa kahawa aina ya Arabika na Robusta,
wakati kipato cha mwanachi ni chini ya dola moja.
Ndadaye aliuawa usiku wa manane nyumbani kwake, miezi mitatu tangu
kuchaguliwa kwake, baada ya chama cha FRODEBU, kujipatia ushindi mkubwa
kilipokibwaga chama cha Watutsi, UPRONA, kilichokuwa madarakani chini ya
uongozi wa Charles Mukasi.
Burundi imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki miaka miwili
iliyopita. Misukosuko ya mauaji makubwa ya kikabila ilianza mwaka 1972 pale
Wahutu waliokuwa wengi jeshini, walipopindua serikali ya Watutsi waliokuwa
wameshika hatamu ya uongozi chini ya rais Michael Michombero ambaye ni Mtutsi.
Kwa sasa mapigano ya kikabila yamepungua lakini zipo taarifa za
chinichini kuwa hali ya mambo si shwari na tayari imezusha hofu kwa wananchi
waliokuwa wamesahau machafuko.
Burundi inatawaliwa kwa kutumia katiba ya mwaka 2005 inayoelekeza
kuwa kutakuwa na uchaguzi wa rais kila baada ya miaka mitano.
Bunge la Burundi lenye viti 100, lina asilimia 60 ya wawakilishi
Wahutu na asilimia 40 ni Watutsi. Asilimia 30 ya wawakilishi bungeni ni
wanawake.
Watutsi ndio waliokuwa wakazi asilia wa Burundi, lakini idadi yao
ilizidiwa na Wahutu. Katika karne ya 15, Watusi waliingia eneo hilo na kuwazidi
nguvu ya kiutawala Wahutu.
Wakati wa vita vikuu vya kwanza vya dunia, majeshi ya Ubelgiji
yaliitwaa Burundi mwaka 1916 na mwaka 1919 nchi hiyo ikawa sehemu ya himaya ya
Ubelgiji.
Julai mosi, 1962, Burundi ilipata uhuru. Lakini katika miaka hiyo ya
1960, ilitawaliwa na mapigano yaliyohusisha Wahutu na Watutsi.
Mwaka 1965 kulitokea jaribio la mapinduzi lililofanywa na Wahutu na
kusababisha Watutsi walipe kisasi kwa kuwaua Wahutu wengi. Julai 1966,
Mwambutsa wa IV alipinduliwa na mwanawe aliyefanywa kuwa Ntare wa V. Naye
alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Novemba 1966.
Michel Micombero, ambaye alikuwa amechaguliwa waziri mkuu mwaka
1966, akawa rais, na katiba mpya ikaanzishwa mwaka 1970.
Micombero naye alipinduliwa na Kanali Jean-Baptiste Bagaza, pia
Mtutsi, ambaye aliimarisha utawala wa Kitutsi madarakani.
No comments:
Post a Comment