AlShabaab yaungana rasmi na al-Qaeda
Kundi la Waislam wenye itikadi kali nchini Somalia,
al-Shabaab, limetangaza kuwa linaungana na kundi la al-Qaeda.
Tamko hilo limetolewa katika picha
ya video iliyotolewa na makundi hayo mawili.
Yusuf Garaad wa Idhaa ya Kisomali ya
BBC ambaye ameitazama video hiyo amesema kundi hilo ambalo jina lake kamili ni
Harakat al Mujahiddin al Shabaab, limetangaza rasmi kuungana na al-Qaeda.
Madai ya muungano huo yametolewa na
kiongozi wa al-Shabaab, Ahmed Godane, au maarufu kama Abu Zubair.
Mkuu
wa al-Qaeda, Ayman al-zawahiri akiwa na Osama
Akizungumza kwa lugha ya Kiarabu,Abu
Zubair amesema sasa watatii maelekezo kutoka kwa kiongozi wa al-Qaeda, Ayman
al-Zawahiri.
Akizungumzia Marekani, Ahmed Godane
amesema wakati wa dola pekee duniani- Marekani - sasa umefikia mwisho na kuwa
utawala wa Uislam ndio utachukua mamlaka.
Kiongozi wa al-Qaaeda, Ayman
al-Zawahiri, ambaye pia ameonekana katika video hiyo, ameisifia al-Shabaab na
kukiri na kukubali kwa kundi hilo kuungana na al-Qaeda.
Amesema hizo ni habari njema kwa
wafuasi wake.
Wapiganaji
Al-Zawahiri amesema Somalia itakuwa
ngome ya Jihad katika pembe ya Afrika na kuongeza kuwa watateketeza kile
alichotaja kuwa ni kiburi cha majeshi ya Kikristo kutoka Marekani, Ethiopia na
Kenya dhidi ya Wasomali.
Ametoa wito kwa al-Shabaab kulinda
watu wake hasa wale ambao ni dhaifu, na pia kutaka kwa wananchi wa Somalia
kuunga mkono uamuzi wa vijana wao, akimaanisha al-Shabaab.
Al-Shabaab ni kundi lenye wapiganaji
maelfu kadhaa, wengi wao wakiwa ni Wasomali. Hata hivyo wanao pia wapiganaji wa
kigeni kutoka katika nchi zinazoizunguka Somalia na hata sehemu nyingine
duniani.
Mitindo yao ya upiganaji ni pamoja
na mabomu ya kujitoa mhanga na pia ya kutegwa ndani ya magari.
Mwenendo
Al-Shabaab kwa sasa inadhibiti
maeneo kadhaa ya kusini na kati ya Somalia.
Katika miezi kadhaa iliyopita
wamekuwa wakibanwa kutoka pande kadhaa. Mjini Mogadishu wanapambana na majeshi
ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, Amisom, yenye wanajeshi kutoka Uganda,
Burundi na Djibouti. Majeshi hayo yanadhibiti zaidi mji mkuu, Mogadishu.
Upande wa kusini, majeshi ya Kenya
yameshambulia ngome za al-Shabaab ardhini, baharini na angani. Majeshi ya
Ethiopia pia yanashambulia kundi hilo kwa upande wa kaskazini na tayari
wameteka mji wa Beled Weyne, mji muhimu katikati mwa Somalia.
Kuungana kwa al-Shabaab na al-Qaeda
huenda kukabadili mwenendo mzima wa mzozo wa Somalia.
chanzo na bbc swahili
No comments:
Post a Comment