KUNA tofauti kati ya maneno
KWELI na U-KWELI, ingawa maneno haya yanatumika mara nyingi kuelezea jambo
moja. Neno kweli linaweza kuwa na ukweli zaidi ya mara moja. Kila mtu anaweza
kuwa na ukweli wake juu ya kweli moja.
Kilicho kweli ni kuwa
Operesheni Tokomeza iliendeshwa, lakini kuna ukweli zaidi ya mmoja, ule
tuliousikia kutoka kwenye Kamati ya Bunge na ule mwingine ambao haujapata
nafasi ya kusemwa au kwa mazingira yalivyo, hausemeki na haupokeleki.
Niweke wazi, naunga mkono
Operesheni Tokomeza na nasikitika kwa matatizo yaliyojitokeza ambayo ni ajali
ya kioperesheni. Ajali ya kioperesheni kama ilivyo ajali ya kikazi inaweza
kutokana na uzembe au hitilafu ya kitendea kazi/mfumo.
Bahati
mbaya suala la Operesheni Tokomeza liliingia hisia na hivyo limezaa hisia. Hata
mjadala wake umejaa hisia kiasi kwamba ukijadili kinyume chake unaonekana wa
ajabu. Hata Profesa nguli kama Issa Shivji naye (katika makala yake toleo la
gazeti hili lililopita) alijadili kwa hisia.
Kamati ya Bunge nayo
walimezwa na hisia na haishangazi waliwasilisha ripoti ile mbele ya Bunge kwa
hisia, wabunge wote wakajadili ripoti hiyo kwa hisia kubwa. Mara nyingi ni
vigumu kushindana na hisia, kwa sababu hisia hazisikii sauti ya mantiki.
Hakuna namna, serikali
ingejitetea, ingefafanua na ikaeleweka, hisia zilikuwa lazima zishinde. Upepo
utakapotulia na hisia zikashuka, mantiki itajitokeza.
Operesheni Tokomeza
inatajwa kuendeshwa kwa namna ambayo imedhalilisha utu na kuminya haki za
binadamu. Operesheni hiyo pia imesababisha mauaji ya 'raia' 13. Neno raia
nimeliweka katika kifungua na kifunga usemi kwa kuwa linapaswa kutumika kwa
tahadhari kubwa. Hali kadhalika, askari sita nao wamefariki katika Operesheni
Tokomeza, hawa hawatajwi wala hawatamkwi, hawaonekani kama nao ni binadamu,
wala hawajadiliwi wameuawa na nani. Kupoteza raia ni jambo kubwa, kupoteza
askari ni jambo kubwa zaidi. Si rahisi kwa askari kufa katika operesheni dhidi
ya raia, isipokuwa tu kama 'raia' nao wanapambana.
Dhana potofu kuhusu
Operesheni Tokomeza
Kuna maneno mawili ambayo
yanatumika bila tahadhari katika suala hili. Neno la kwanza ni 'operesheni' na
neno la pili ni 'raia'. Kwanza, operesheni ni mapambano dhidi ya hatari fulani.
Operesheni ni 'ama zao-ama zetu' na kawaida huambatana na athari (damages) kwa
kuwa inaendeshwa dhidi ya kikundi au adui ambaye naye ana nguvu.
Kutangaza operesheni
maana yake ni kuwa hatari iliyopo haiwezi kudhibitiwa kwa mbinu na medani za
kawaida za ulinzi na usalama. Isitoshe, aina ya silaha na kikosi, inategemea
sana na aina ya tishio na makisio ya uwezo wa adui mwenyewe.
Kinachofanya operesheni
kuitwa ya mafanikio, ni pale inapofikia lengo na inapokuwa na athari ndogo
ikilinganishwa na lengo lililofikiwa. Kwa kifupi, mafanikio ya operesheni
hayamaanishi kuwa hakuna madhara, bali madhara ni madogo kuliko faida.
Neno la pili ambalo
linatumiwa vibaya ni 'raia'. Dhana inayojengwa hapa ni kuwa raia wote ni wema
wakati wote, na kuwa majangili si raia. Kwa haraka haraka, tunaaminishwa kuwa
Operesheni Tokomeza ililenga majangili na si raia ambao ni majangili. Majangili
hawa wamejitenga mbali na raia, wanaishi mahala fulani wamekusanyika ambako
vikosi vya operesheni vilitakiwa vikawakute huko na kupambana nao, na si
kuwatafuta miongoni mwa raia.
Tunachojisahaulisha ni
kuwa, taarifa za kukamatwa kwa meno ya tembo zimeonyesha majangili hawa
wakikamatiwa majumbani kwa raia wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa,
wanawake, wanaume na hata watumishi wa umma na vyombo vya dola. Kwa mlinganyo
huu, ni vigumu kutenganisha raia mwema na jangili, pia inakuwa vigumu wigo wa
mapambano kuishia porini pekee bila kuendesha operesheni uraiani.
Mantiki na haja ya
operesheni
Ilipotangazwa Operesheni
Tokomeza wabunge, wananchi na wadau wa uhifadhi na mazingira walifurahia.
Walifurahi kwa kuwa wote waliguswa na kasi ya kutisha ya ujangili uliokuwa
ukiendelea nchini. Inakadiriwa kuwa Tanzania imepoteza nusu ya idadi ya tembo
wake katika kipindi cha muongo mmoja. Taarifa za kukamatwa shehena mbalimbali
za meno ya tembo zilikuwa zimezizima na mbaya zaidi zikihusisha hata askari
wasio waaminifu kukamatwa na meno hayo wakitumia magari ya serikali.
Kulikuwa na kilio kote
nchini cha kulaumu serikali kwa kutochukua hatua. Tena, ikumbukwe kuwa umma
ulitaka serikali kuchukua hatua kali, ndio maana haishangazi kuwa umma
ulifurahia habari za kuanzishwa kwa Operesheni Tokomeza bila hata kutaka kujua
itaendeshwaje. Walichoshwa na ujangili kuliko kujali madhara yatakayotokana na
operesheni. Pengine kutokana na kugubikwa na hisia, hawakufikiria ama walisahau
kuwa operesheni ni mapambano na sio lelemama.
Shinikizo kubwa
lilikuwepo kutoka nje ya nchi. Jumuiya ya Kimataifa ilitaka kuona Tanzania
ikichukua hatua. Suala hili la ujangili lilizungumzwa na Rais Barack Obama
alipokuja nchini. Mikutano kadhaa iliitishwa duniani wakitaka kuona Jumuiya ya
Kimataifa ikiungana kudhibiti ujangili. Ilishtua zaidi, pale ilipogundulika
kuwa, mtandao huu wa ujangili ni wa kimataifa na unahitaji ushirikiano wa
kimataifa kukabiliana nao. Jumuiya ya Kimataifa nayo ilipokea kwa furaha
taarifa za Tanzania kuanzisha Operesheni Tokomeza ujangili. Kwa ufupi, wakati
ulikuwa muafaka na lengo lilikuwa muafaka. Hapakuwa na mbadala zaidi ya
serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza.
Maandalizi na utekelezaji
wa Operesheni
Kimsingi, kunakodaiwa
kufeli kwa Operesheni Tokomeza kunaonekana katika maandalizi na utekelezaji wa
operesheni na si mantiki ya kuanzishwa kwake. Nikiri awali kuwa taarifa za
maandalizi na utekelezaji wa operesheni ni taarifa za siri ambazo haziko wazi
kwa umma. Hata Kamati ya Bunge imekiri kuwa mchakato mzima ulikuwa ukiendeshwa
kwa usiri. Ukweli huu, hautuzuii kung'amua matatizo yanayoweza kuchangia
kunakoitwa kufeli kwa operesheni hii madhali sasa taarifa za kutosha za
operesheni hiyo zimetoka nje.
Kinachoonekana haraka
haraka ni kuwa inawezekana kuwa kulifanyika makosa katika ukusanyaji wa taarifa
za uchunguzi wa nani hasa wanahusika na mtandao huo.
Haifahamiki vizuri ni kwa
kiasi gani kamati za usalama za wilaya na mikoa zilihusishwa, na pale
zilipohusishwa zilichangia kwa kiasi gani katika umakini wa taarifa zao za
uchunguzi. Taarifa za kamati hizi za usalama za wilaya na mikoa ni muhimu kwa
kuwa huko ndiko ujangili unakotendeka. Hata hivyo, changamoto kubwa ni kuwa,
kamati hizi pengine hazikuwa za msaada sana kwa kuwa wajumbe wa kamati hizi,
baadhi ni washiriki au wafaidikaji wa mtandao wa ujangili.
Tatizo jingine kubwa
linaloweza kuchangia upungufu wa Operesheni Tokomeza ni operesheni zingine
zilizokuwa zikiendelea dhidi ya wafugaji. Itakumbukwa katika Bunge la Oktoba,
2013 kuliibuka mjadala mkali kutoka kwa wabunge wanaowakilisha maeneo ya
wafugaji juu ya wafugaji kuonewa kwa kuzuiliwa malisho ya mifugo yao.
Tayari uhusiano kati ya
wafugaji na wakulima ulikuwa umekwishasababisha maafa na chuki za kijamii.
Serikali za vijiji, wilaya na mikoa nazo zilikuwa lawamani kwa kushindwa
kudhibiti migogoro hii, na wakati mwingine zikituhumiwa kutoa upendeleo, hasa
kwa wakulima kutegemeana na wapi serikali hizo zipo, kwa maana ya maeneo ya
wakulima wengi au wafugaji wengi.
Hivyo, haitii shaka kuwa,
baadhi ya watendaji wa ngazi za vijiji, wilaya na mikoa waliiona Operesheni
Tokomeza kama mwanya wa kutokomeza tatizo la wafugaji wa kuhamahama,
waliopachikwa jina la 'wafugaji haramu'. Ndio maana, tunakuta katika Operesheni
Tokomeza Ujangili wanauwawa wafugaji na mifugo.
Kuna uwezekano kuwa baadhi
ya sehemu taarifa zilipotoshwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya kutokana na
wajumbe kuwahisi tu baadhi ya watu kuwa ni majangili au wanahusika nao.
Matatizo kama haya yalijitokeza pia wakati wa operesheni dhidi ya biashara ya
viungo vya albino. Pengine, uharaka wa kufanikisha operesheni hiyo ulitokana na
shinikizo la ndani na nje ya nchi bila kutoa muda wa kutosha wa maandalizi.
Hali kadhalika, matatizo haya inawezekana yametokana na udhaifu wa kiuratibu
kwa vile operesheni ilihusisha wizara tatu.
Pengine, upungufu ama
udhaifu huo, uliwalazimu waendesha operesheni kutumia mbinu ya kutesa ili
kukusanya taarifa zaidi. Kwa ufupi, mbinu hii ya utesaji ni kielelezo cha
kukosekana kwa weledi katika maandalizi na ukusanyaji wa taarifa.
Kwa kiasi kikubwa, ufanisi
wa operesheni unategemea ukamilifu wa maandalizi ya mezani kabla ya kufika
uwanjani. Kwa maelezo yoyote yale, kama operesheni inasemwa kuwa imefeli, basi
kufeli huko lazima kutokane na upungufu katika maandalizi na utekelezaji.
Operesheni kusitishwa kabla
kukamilishwa
Tutakumbuka kuwa
Operesheni Tokomeza ilisitishwa mapema tu baada ya kuanza kwake. Kusitishwa
huko kulitokana na vilio vya wabunge na kulizaa Azimio la Bunge la kuunda
kamati ndogo ya Bunge, kuchunguza na kutoa taarifa na mapendekezo bungeni.
Wakati operesheni hiyo
inasitishwa, takwimu zilionyesha kuwa askari sita na raia 13 waliuawa na
kulikuwepo kesi 687 na watuhumiwa 1,030 na meno ya tembo 706 yalikamatwa,
ambayo ni sawa na tembo 353 waliouawa. Takwimu hizi ni vyema zikazingatia kuwa
operesheni hii imedumu kwa siku zisizozidi 28, yaani kuanzia Oktoba 5
hadi Novemba mosi, 2013.
Binafsi napata taabu sana
kusema kuwa Operesheni Tokomeza imefeli. Napata taabu zaidi kuelewa vigezo
vinavyotumiwa na wale wanaosema operesheni imefeli. Ni vigumu kusema operesheni
imefeli wakati haikumalizika baada ya kusitishwa katikati.
Pia, takwimu za idadi ya
watuhumiwa, kesi na meno ya tembo yaliyokamatwa kwa kipindi hicho, hayashawishi
kusema kuwa operesheni imefeli. Isitoshe, katika kipindi hicho, hata baada ya
operesheni kusitishwa, taarifa za matukio ya ujangili hazisikiki au zimepungua
sana. Ni vigumu kubisha kuwa operesheni hii imeshitua majangili ama
ilisambaratisha mtandao wao kwa kiasi kikubwa.
Tayari, ziko sauti
zinazotahadharisha kuwa kusitishwa huku kwa operesheni kunatoa mwanya kwa
majangili kujipanga upya, pia zipo sauti za kusema operesheni iendelee
isipokuwa isimamiwe vizuri zaidi.
Binadamu ni viumbe wa
hisia. Hisia moja hufunika nyingine. Hisia zilizoamshwa na vifo na madhila
yaliyowafika baadhi ya raia ambao hatujui kama walikuwa ni raia wema, majangili
au washirika wa majangili zimegubika faida na matokeo yote chanya ya operesheni
hii. Operesheni yote imeonekana mbaya na ya kikatili. Historia inatufundisha
kuwa hata katika Operesheni Vijiji vya Ujamaa, kulikuwepo malalamiko makubwa ya
ukiukwaji wa haki za binadamu ingawa unaweza usifikie huu wa sasa. Leo,
tunaishi matunda ya Operesheni Vijiji vya Ujamaa, tunajenga shule, zahanati
kila kijiji na sasa tunapeleka umeme vijijini kwa kuwa vijiji vipo.
Msingi wa hoja hapa ni
kuwa, Operesheni Tokomeza haikufeli kabisa. Ni vigumu kusema pia ilikuwa na
mafanikio makubwa na mazuri. Kama nilivyosema awali, mafanikio makubwa ya
operesheni yoyote ni pale ambapo imeendeshwa kwa ufanisi kiasi cha kutokuwa au
kuwa na madhara madogo yasiyotarajiwa. Operesheni Tokomeza haikupewa muda wa
kutekeleza vya kutosha kiasi cha kuweza kupima uwiano kati ya matokeo na
madhara, pengine mwishowe pangelikuwepo na mafanikio makubwa sana kuliko
madhara.
Hali kadhalika, mtu
mwingine angeweza kusema kuwa operesheni hii ingeendelea madhara yake yangezidi
mafanikio. Majumuisho yote haya yana mantiki kwa kuwa operesheni ilisitishwa
njiani. Tunachoweza kusema ni kuwa Operesheni Tokomezo ilikuwa na mseto wa
mafanikio, madhara na mafunzo mengi kwa taifa letu.
Hatua za uwajibikaji
Uwajibikaji hauepukiki
katika Operesheni Tokomeza hata kama ingekuwa ya mafanikio. Operesheni hii kwa
asili ilikuwa iambatane na gharama za kisiasa. Operesheni Tokomeza haikuwa
operesheni ya kawaida, kiwango cha tishio na hatari iliyoletwa na ujangili
kuliifanya operesheni hii kuwa ya kufa au kupona. Adui hakuwa wazi maana hakuna
jeshi la majangili, adui huyo amejificha miongoni mwa raia tena wakati mwingine
katika kivuli cha mwanasiasa, mtendaji, mfanyabiashara na hata mwanamke.
Ilikuwa vigumu kwa hali yoyote kuepuka kudhuru raia mwema, ambacho
kingewezekana tu ni kudhibiti madhara hayo kuwa madogo sana kwa kutumia mbinu
za kisayansi, kiintelijensia na medani za juu za kivita.
Napata taabu kukubaliana
na wale wanaosema kuwa serikali isingetumia jeshi au kutobughudhi raia. Katika
washiriki 2,371, wanajeshi walikuwa 885 au asilimia 37. Polisi walikuwa 480 au
asilimia 20 tu. Napata taabu kwa kuwa, tayari kikosi cha wanyamapori
kilishaelemewa na majangili. Takwimu zinaonyesha kuwa, askari wanyamapori 1,000
wamepoteza maisha Afrika mwaka jana, wakipambana na ujangili kwa kuwa majangili
hawa wana mafunzo ya kijeshi na wanatumia silaha nzito.
Aidha, hatuna polisi wa
kutosha wa kujazia asilimia 37 ya nguvu kazi ya wanajeshi walioshiriki
Operesheni Tokomeza bila kuathiri uwezo wa Jeshi la Polisi kuendelea na
majukumu yake ya kila siku ya usalama wa raia na mali zao. Ikumbukwe kuwa Jeshi
la Polisi tayari lina lawama nyingi ikiwa ni pamoja na askari wachache
ukilinganisha na mahitaji makubwa ya nchi. Sioni njia nyingine ambayo serikali
ingetumia zaidi ya kutumia sehemu ya jeshi, kinyume cha kufanya hivyo,
ingelazimu serikali kukodisha polisi nje ya nchi, jambo ambalo kiusalama
halileti mantiki. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina wajibu na jukumu la
kulinda nchi wakati wa vita na wakati wa amani.
Taharuki iliyoikumba
serikali inaweza kuelezewa vyema na simulizi ya Jenerali Wojciech Jaruzelski,
Mtawala wa Poland aliyoitoa mwaka 1981 akiwa ughaibuni akilaumiwa kwa mauaji makubwa
yaliyotokea baada ya yeye kutangaza hali ya hatari iliyosababisha wanajeshi
kuingia mtaani kudhibiti usalama.
Alipoulizwa na mwandishi
baadaye, baada ya kustaafu ni kwa nini alitoa uamuzi wa hali ya hatari
uliosababisha maafa makubwa, alijibu ifuatavyo: "Nimeshahukumiwa na
magazeti, lakini napenda kuwakumbusha wanahistoria uchwara kuwa, si mimi
niliyeumba mazingira ya historia yaliyokuwapo. Historia ilinifikisha katika
hali ambayo sikuwa na jinsi zaidi ya kuchagua baina ya machaguo mabaya mawili
(sio chaguo moja baya na jingine zuri). Uchaguzi wowote ambao ningeufanya
ungekuwa na matokeo mabaya, nilikuwa katika wakati mgumu, mimi ni mzalendo
siwezi kuitwa muuaji, kwa kuchukua uamuzi ule wa kutangaza hali ya hatari,
niliiokoa Poland kutoka kwenye hatari kubwa zaidi".
Mazingira aliyofanyia
uamuzi Jenerali Jaruzelski yanafanana na mazingira ambayo serikali ilifikishwa
katika kuamua kuanzisha Operesheni Tokomeza. Serikali ilikuwa na machaguo
mawili tu nayo yote yalikuwa yaishie kwenye kulaumiwa.
Ilikuwa ni aidha uache
tembo watokomee ulaumiwe, au upambane na ujangili ulaumiwe. Kupambana na
ujangili ilikuwa ndio chaguo lenye afadhali kati ya machaguo hayo mawili.
Hatimaye, serikali ingeishia kuwajibika.
Nawapongeza mawaziri
waliowajibika kwa niaba ya serikali, nampongeza zaidi Rais Jakaya Kikwete kwa
kuwakubalia kufanya hivyo. Angeliweza kukataa na anayo mamlaka ya kufanya
hivyo. Serikali ingeweza kutaka kujitetea juu ya kilichotokea na pengine
ingeilazimu serikali kutoa taarifa za kiusalama ambazo si busara zitolewe
hadharani.
Kuwajibika kwa serikali
kuna maana ya kukiri udhaifu na madhara yaliyojitokeza, kuelezea masikitiko
yake kwa wale walioathirika, kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza na
kurejesha imani kwa wananchi juu ya serikali.
Tunaelekea wapi baada ya
hapa?
Serikali pamoja na mambo
mengine imechaguliwa iongoze, iamue na itekeleze. Serikali haiwezi kukwepa
kulaumiwa katika kutekeleza wajibu huo. Mamlaka ya juu kabisa katika nchi yenye
dhamana juu ya watu, uhai na mali zao ni serikali, hivyo lazima ilaumiwe pale
uhai na mali za watu zinapopotea aidha kutokana na serikali kutotenda au
kutenda. Serikali ililaumiwa kwa kutopambana na ujangili na mtandao wake
unaowahusisha wafanyabiashara na wanasiasa, hali kadhalika imelaumiwa kwa
kupambana na mtandao huo.
Operesheni Tokomeza
imetufundisha mengi tuliyoyajua na ambayo hatukuyajua. Kama nilivyosema,
operesheni hii haikuepukika, na labda ilipaswa kutokea ili kutushitua kuhusu
udhaifu wa kimfumo na kimuundo uliokuwapo.
Pengine,
pasingekuwapo na Operesheni Tokomeza, tungekuja siku moja kugutushwa na janga
kubwa zaidi. Wachina wana msemo wao kuwa "kila janga huja na fursa
zake". Ni wakati sasa wa kuangalia fursa zitokanazo na majanga
yaliyotokana na operesheni hii. Operesheni Tokomeza inatupa mafunzo kadhaa.
Mosi, operesheni si njia
nzuri ya kutatua matatizo na yatupasa sasa kujenga tabia ya kuyakabili matatizo
yakiwa bado madogo kabla hayajaota mizizi na kuhitaji operesheni. Hivi sasa
liko janga la dawa za kulevya, na hili la wafugaji na wakulima. Hali inavyokwenda
kama hayatadhibitiwa, itatulazimu operesheni siku za usoni na serikali
italazimika kuwajibika.
Pili, Operesheni Tokomeza
imetufundisha udhaifu mkubwa ulioko katika mifumo ya serikali ngazi za wilaya
na mikoa, hususan kamati za usalama. Huko nako kunahitaji kusukwa upya na
kuimarisha mfumo wa utawala. Laiti wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wabunge
wangefanya kazi vizuri, tusingefikishwa hapa. Tumefikishwa katika operesheni
kwa kuwa ngazi za wilaya na mikoa zilielemewa ikalazimu kunusuriwa kitaifa,
yaani operesheni. Migogoro ya wakulima na wafugaji na ulinzi na usalama
wilayani na mikoani unahitaji uratibu na uongozi kwanza, silaha baadaye.
Tatu, Operesheni Tokomeza
inatuamsha kufanya tathmini na kuboresha uwezo wa vikosi vyetu vya ulinzi na
usalama kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama. Uhalifu unapanuka duniani
kote na unajiimarisha kiteknolojia, kiintelijensia na kimtandao. Majeshi yetu
nayo yanapaswa kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko haya. Tunahitaji kuongeza
uwezo wao wa kufanya operesheni za ndani ya nchi, na muhimu ushirikiano kati ya
majeshi ya ulinzi na usalama katika kutekeleza majukumu yao. Ni vyema
tukawekeza katika kuyawezesha majeshi yetu nchini kufanya mazoezi na mafunzo ya
pamoja hususan katika kukabili majanga. Muhimu zaidi, kuyaelimisha zaidi juu ya
wajibu wao kwa raia na kurejesha imani yao kwa wananchi ambayo imeporomoka
sana.
Nne, operesheni tokomeza
inakumbusha serikali juu ya kuhimiza wajibu wa wananchi katika ulinzi wa nchi
yao. Serikali imeacha kuhimiza na kuelimisha umma juu ya wajibu huu. Pale
wananchi wanapowajibika katika ulinzi na usalama wa nchi, wahalifu wakiwemo
majangili hawawezi kutufikisha hatua ya operesheni. Sote tunafahamu, majangili
hawaishi porini, wanaishi miongoni mwetu, tunakula nao, tunakunywa nao na
kuishi nao. Wananchi wanapaswa kuwafichua na kushirikiana na dola kuwatokomeza.
Kinyume cha hapo, majangili na wahalifu watawaponza raia wema pale operesheni
itakapopita, maana itawia vigumu kutofautisha raia na jangili.
Aliwahi kusema Wiston
Churchil, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kuwa, "Mataifa na watu wake
hupata busara baada ya kumaliza fursa zote". Tukijenga utamaduni wa
kutumia fursa za kurekebisha maovu mapema, hatutalazimika kuja kung'amua busara
baada ya kuwa tumedhurika, kama ilivyotokea kwa Operesheni Tokomeza.
- CHANZO:
http://www.raiamwema.co.tz/hisia-hazisikii-sauti-ya-mantiki
No comments:
Post a Comment