Jenerali wa Marekani, Norman
Schwarzkopf, ambaye aliongoza majeshi ya Marekani na ya ushirika yaliyoyatoa
majeshi ya Iraqi kutoka Kuwait mwaka 1991 amefariki mjini Tampa,
Marekani.
Jenerali Schwarzkopf ndiye
aliyeongoza vita ya Ghuba (Operation Desert Storm) ambayo ndio ilisaidia
kuikomboa Kuwait kutoka kwa Dikteta wa Iraqi, Saddam Hussein mwaka 1991,
amekufa akiwa na umri wa miaka 78.
Schwarzkopf maarufu kama
"Stormin' Norman," amefariki kutokana na matatizo ya nimonia akiwa
Tampa, ambapo alistaafu akiwa na cheo cha Kiongozi Mkuu wa Kamandi ya Kati ya
Marekani.
Rais wa zamani wa Marekani, George
H. W. Bush, ambaye naye amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa walio kwenye
uangalizi maalumu mjini Texas, alikuwa wa kwanza kutoa salamu za msiba kwa kifo
cha kamanda huyo ambaye ndiye alimchagua mwenyewe kuongoza vita ambayo
iliwaweka kwenye chati wote wawili.
"Barbara na mimi tunaomboleza
kwa kumpoteza shujaa halisi wa Marekani na mmoja wa kiongozi mahiri wa jeshi
katika kizazi chake,” alisema.
Wakati wa vita ya kuikomboa Kuwait,
Jenerali Schwarzkopf aliongoza askari 425,000 wa Marekani ambao waliungana na
wanajeshi 118,000 wa ushirika kutoka mataifa mengine na kufanikiwa kuharibu
mashine za vita za Saddam na kumtoa Kuwait bila kumng’oa madarakani.
Jenerali Schwarzkopf alizaliwa
Trenton, New Jersey mwaka 1934.
No comments:
Post a Comment