MMOJA wa wanasiasa
waliotoa mchango mkubwa katika kudai uhuru wa Malawi, Kanyama Chiume (78),
amefariki dunia.
Kifo cha Kanyama Chiume,
ama kwa jina kamili, Murray William Kanyama Chiume, ambaye alifariki dunia
mjini New York, Marekani Jumatano iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu,
kimegusa watu wengi sehemu mbali mbali duniani, pamoja na Tanzania
ambako alisoma na kuishi kabla ya kurudi Nyasaland kuungana na wanaharakati
wenzake kudai uhuru.
Hata hivyo, historia ya
mwanasiasa huyo mkongwe katika siasa za Malawi ni sawa na hadithi ya tingatinga
ambalo baada ya kutumika kiasi cha kutosha kama kifaa muhimu katika ujenzi wa
barabara nzuri, barabara hiyo inapomalizika ‘linapigwa marufuku’ kutumia
barabara hiyo eti litaiharibu.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa
kwa Chiume. Baada ya nchi hiyo kupata uhuru Julai 6, 1964 na jina lake
kubadilishwa kuwa Malawi, Chiume na wenzake kadhaa waliokuwa mawaziri wa Malawi
huru walitofautiana na Rais wao, Prezidenti wa Muyaya, Ngwazi Dk Hastings
Kamuzu Banda, kuhusiana na masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na hatua ya Rais huyo
kuwakumbatia makaburu wabaguzi wa rangi wa Afrika Kusini na Wareno waliokuwa
wanatawala Msumbiji kimabavu.
Chiume, mawaziri wenzake
pamoja na ndugu zao wakajikuta na wakati mgumu baada ya kukorofishana na Banda.
Walilazimika kuikimbia nchi hiyo na yeye alikuwa miongoni mwa waliokimbilia
Tanzania kuishi kama wakimbizi wa kisiasa.
Hakurudi Malawi hadi
mwaka 1994 wakati Banda alipobanwa na kulazimishwa kuendesha kura ya maoni
ambayo ilionyesha ya kuwa Wamalawi walio wengi wanataka nchi yao iwe na mfumo
wa vyama vingi vya siasa na si chama kimoja kama Banda alivyokuwa
anang’ang’ania.
Akiwa uhamishoni
Tanzania, Chiume alipata kufanya kazi kwenye magazeti ya Uhuru, Nationalist
(limekufa), Daily News na Sunday News. Alikuwa pia akiandikia majarida maarufu
ya nje yaliyokuwa yakichapishwa London makala kuhusu hali halisi ya Malawi
chini ya utawala wa Banda.
Chiume ambaye
alizaliwa Usisya, Wilaya ya Nkhata Bay, Nyasaland, Novemba 1929, alijiingiza
katika siasa kwenye miaka ya 1950 na kuendelea kushikamana na wenzake kudai
uhuru hadi ukapatikana.
Kama mwanaharakati wa
kudai uhuru, Machi 1959, akiwa na umri wa miaka 29, Chiume alisalimika
kukamatwa kutokana na kuwa ziarani Mombasa, Kenya, baada ya wakoloni kutangaza
hali ya hatari.
Viongozi wenzake wote wa
chama chao cha Nyasaland African Congress waliokuwapo Nyasaland wakati huo,
walikamatwa na kupelekwa katika magereza ya Rhodesia ya Kusini (sasa
Zimbabwe) na chama kikapigwa marufuku.
Orton Chirwa aliyekuwa
miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kuachiwa huru Rhodesia na kurudishwa
nyumbani, alianzisha chama kipya cha Malawi Congress Party, baadaye aakajivua
Urais na kumkabidhi Kamuzu Banda. Ni chama hicho ambacho baadaye
kilifanikisha kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo.
Katika harakati za kudai
uhuru, Julai 1960 Chiume aliungana na Banda, Chirwa na Aleke Banda kwenye
Mkutano wa Katiba wa Nyasaland mjini London, Uingereza. Ilikuwa kwenye mkutano
huo ambako Serikali ya Uingereza ilipoamua Nyasaland ijitawale
ifikapo mapema 1963, kwa hiyo Banda mwaka 1962 akawa Waziri Mkuu huku Chiume
akiwa Waziri wa Elimu, lakini baadaye akawa Waziri wa Mambo ya Nje katika
serikali ya kwanza baada ya uhuru.
Chiume alikuwa
kiongozi muhimu katika mgogoro wa Baraza la Mawaziri mwaka 1964. Alitajwa
kama kiongozi wa mgogoro huo na adui namba moja wa Banda. Pamoja na msimamo
wake usiotetereka wa kusimamia maslahi ya wanyonge na umoja wa Afrika, Banda
hakupendezwa na hotuba aliyokuwa ameitoa katika mkutano wa Umoja wa Nchi Huru
za Afrika mjini Cairo, Misri.
Baada ya mgogoro wa
Baraza la Mawaziri kuibuka, Banda aliwafuta kazi za uwaziri Kanyama Chiume
(Waziri wa Mambo ya Nje na Habari), Orton Chirwa (Waziri wa Sheria) na Harry
Bwanausi (Waziri wa Maendeleo na Nyumba). Saa chache baadaye, Yatuta Chisiza
(Waziri wa Mambo ya Ndani) na Willy Chokani wakajiuzulu kuonyesha mshikamano na
wenzao. Chipembere (Waziri wa Elimu) ambaye alikuwa ziarani Canada wakati huo
alirudi nyumbani na kutangaza na yeye kubwaga manyanga.
Malawi ikawa nchi
isiyokalika kwa mawaziri ‘wakorofi’ na ndugu na marafiki zao. Henry Chipembere,
Orton Chirwa na Yatuta Chisiza wakakimbilia Tanzania. Mwaka 1969, Chisiza
aliuawa kwa kupigwa risasi baada ya jaribio lake la kuingia Malawi akitokea
Tanzania na wafuasi wake kugundulika. Chipembere aliondoka Tanzania kwenda
kuishi Marekani ambako alifariki.
Kuna jambo moja ambalo
pengine vizazi vya sasa vya Malawi vinaweza kuwanyooshea vidole vya lawama
Chiume na wenzake kwamba wanahusika kwa kiasi kikubwa na mateso ambayo wananchi
wengi wa Malawi wameyapitia katika utawala wa mabavu wa ‘Rais wa Maisha,’
Kamuzu Banda.
Hiyo ni kwa sababu
Chiume, Henry Masauko Chipembere na Dunduzu Chisiza ndio hasa waliomkaribisha
Dk. Banda Nyasaland kutoka Uingereza ili awaongoze kudai uhuru. Banda alikuwa
ametokomea Uingereza kwa zaidi ya miaka 40 akijishughulisha na kazi yake ya
udaktari baada ya kumaliza kusoma.
Nini hasa
kiliwatuma Chiume na wenzake kumwita Banda wakati wenyewe walikuwa ni
wasomi wa kutosha? Kwa mfano, Chiume mwenyewe alikuwa amemaliza kusoma Chuo
cha Makerere, Uganda, Dunduzu Chisiza alikuwa msomi wa masuala ya uchumi na
Orton Chirwa alikuwa amebobea katika masuala ya sheria.
Kwa mujibu wa Chiume
(kama nilivyohojiana naye miaka kadhaa iliyopita Dar es Salaam) ilikuwa ni
muhimu kwa wakati huo kuwa na umoja wa dhati dhidi ya ukoloni wa Uingereza. Na
utamaduni wa Waafrika unaotoa nafasi kwa wazee kuheshimika kwa busara
zao ndio uliowafanya wamwite.
Banda akiwa mzee wa miaka
zaidi ya 60 na usomi wake ni vitu viliyoonekana kuwa silaha kubwa katika kuleta
umoja ambao ungeuangusha ukoloni Nyasaland.
Wakati Nyasaland inapata
Uhuru, Banda alikuwa na umri wa miaka 66, Chiume alikuwa na miaka 35, Yatuta
Chisiza (38), Bwanausi (34), Chipembere (34) na John Tembo (Waziri wa
Fedha) alikuwa na miaka 31.
Lakini dalili kwamba
Banda ni kiongozi matata zilijitokeza hata kabla ya uhuru kupatikana.
Kitabu kuhusu maisha ya Banda kilichoandikwa na Phillip Short kinamnukuu
Chipembere akisema:
“Kulikuwa hili la….
hasira za Dk Banda kuzichukulia maanani. Chochote ukimlaumu alikuwa
anakuja juu vibaya sana kiasi cha kukufanya ufikirie nafasi yako
kama kiongozi. Usingependa kufukuzwa ujumbe wa Kamati Kuu katika Chama au
kupoteza uwaziri na kikubwa usingependa kuwa chanzo cha mgawanyiko kwa wakati
huo.
“Yeyote aliyejaribu
kugombana na Dk. Banda kwa sababu yoyote kabla ya uhuru
kupatikana angechukiwa na wananchi. Ungeweza kupigwa mawe. Kila mtu
alikuwa anasema ‘hebu tuungane, tufanye kazi pamoja, hebu sote tuwe nyuma ya
Dk. Banda ili tupate uhuru wetu. Tusijenge mazingira ambayo yatafanya Serikali
ya Uingereza kuwa na sababu ya kutucheleweshea uhuru…
“Kulikuwa na huyu (Roy)
Welesky (Gavana wa kikoloni wa Nyasaland) ambaye alikuwa tayari kutumia kwa
faida yake matatizo yoyote yanayojitokeza kwenye chama. Ingawa miongoni mwetu
tulishindwa kumlaumu Dk. Banda kutokana na kukosa ushujaa wa kufanya hivyo au
kwa kuhofia matokeo ya hatua atakazochukua kwa kufanya hivyo, kulikuwa na hili
pia la kuhofu kuwapo kwa mgawanyiko kabla ya uhuru. Mnaweza mkakosana baada, si
kabla ya kupatiwa uhuru.”
Na hicho ndicho hasa
kilichotokea. Septemba, miezi mitatu tu baada ya uhuru, walikosana na Dk.
Banda, Chiume akilazimishwa kufanya makazi yake Dar es Salaam ambako hakukaa
bure. Alikuwa mwandishi wa vitabu na aliandika vitabu vya, Banda's
Malawi: Africa's Tragedy mwaka 1992, Kanyama Chiume Kwacha (kuhusu maisha yake
mwaka 1982), The African Deluge (1978), Caro nchinonono (Dunia Ngumu kwa
lugha ya Kitumbuka), Mwana wa Ngoza (Mtoto wa Mwanasesere kwa Kitumbuka),
Dunia Ngumu (kwa Kiswahili), Mbutolwe mwana wa Umma (kwa Kiswahili), Nyasaland
Speaks: An appeal to the British People (1959) na Nyasaland demands secession
and independence: An appeal to Africa (1959).
Uwezo wake mkubwa wa
kuandika, si tu ulimfanya aandike vitabu, ulimpatia kazi kwenye vyombo vya
habari vya Tanzania na kuandika uozo wote uliokuwa ukifanyika Malawi kwa
kutumia majarida maarufu ya nje yaliyokuwa yakichapishwa London, Uingereza.
Marafiki waliokuwa ndani
ya Malawi walikuwa wakimpatia Chiume hali halisi ya utawala wa Banda na yeye
bila woga alianika uovu huo kwa dunia nzima kutambua kinachoendelea nchini
humo. Jambo hilo lilikuwa linamwudhi mno Dk. Banda kiasi alilizungumzia katika
kila mikutano ya hadhara akimwita Chiume kuwa ni mtu hatari.
Marafiki walimwezesha
Chiume kupata picha kamili ya hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya
Malawi na marafiki hao wengi wao wakiwa Wazungu, walimsaidia pia
kufikisha ujumbe wake kwa watu anaotaka uwafikie ndani ya Malawi. Kwa nini
Wazungu? Aliwatumia watu hao kwa sababu ya kuabudiwa mno nchini humo. Ni
pekee ambao walikuwa hawapekuliwi wanapoingia na kutoka nchini humo.
Aliwatumia pia marafiki
hao hata kufikisha ujumbe kwa Banda mwenyewe kwa njia mbali mbali. Hiyo
ilimfanya Banda ataharuki na kujenga picha ya Chiume kama ‘mchawi’ au mtu
mwenye nguvu zisizo za kawaida.
Akiwa na kumbukumbu
ya jinsi waziri wake wa zamani wa Mambo ya Ndani, Yatuta Chisiza alivyoingia
Malawi ‘kivita’ na kikosi kidogo cha wafuasi wake na kupambana na majeshi
ya serikali kabla ya kuuawa, Banda alikuwa pia akihofu Chiume kufanya hivyo.
Aliona salama yake ni
kumtisha katika mikutano ya hadhara kwamba akiingia Malawi itakuwa kiama chake.
Hadi kufikia mwaka 1994, jina la Kanyama Chiume lilikuwa bado linatisha Malawi
karibu sawa na linavyotisha jina la Osama Bin Laden Marekani. Wakati Bush
anamwita Osama kama gaidi namba moja, Banda alikuwa anamwita Chiume kama
‘Chigewenga’ (haramia) namba moja nchini humo.
Lakini Wamalawi ambao
walikuwa wadogo mwaka 1964 wakati Nyasaland inakuwa huru au waliozaliwa baada
ya mwaka huo, walishikwa na butwaa walipomwona Kanyama Chiume Malawi kwa mara
ya kwanza mwaka 1994 akiwa mzee wa kawaida kabisa.
Hakuwa mtu wa miraba
minne, alikuwa hapayuki ovyo na hakuonyesha makeke yoyote mbali ya
kutambulisha chama chake na kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu.
Alikiingiza chama chake
cha Congress for Second Republic (CSR) katika kinyang’anyiro cha kwanza cha
uchaguzi wa vyama vingi, uchaguzi ambao ulimwondoa Banda kwenye madaraka na
kumwingiza Bakili Buluzi na chama chake cha United Democratic Front (UDF).
Chiume akakiunganisha chake na UDF.
Rais Muluzi baadaye
alimteua Chiume kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Maktaba na baada ya kujiuzulu nafasi
hiyo alifungua klabu yake ya kitalii Nkhata Bay aliyoiita Banana Groove.
Pengine kutokana na hadithi zile zile za alinacha za Banda kuhusu Chiume,
miongoni mwa umaarufu wa klabu hiyo ni mchapo wa miongini mwa watu wa kawaida
Nkhata Bay kwamba Chiume alikuwa amepanda mgomba kwenye mwamba.
Ukweli ni kwamba
klabu hiyo ilikuwa ufukweni mwa Ziwa Nyasa na kujengwa kwa mandhari ya
kiutamaduni ilikuwa na migomba kwenye kiunga cha mawe. Hapakuwa na
ajabu hiyo inayoelezwa leo baada ya Chiume kuondoka Malawi na klabu hiyo kuungua
moto katika hali ya utatanishi.
Baadaye Chiume aliamua
kwenda Marekani kwa wanawe ambako mauti yakamfika Novemba 21 mwaka huu.
Ingawa kulikuwa na
maombi ya watu wengi kwamba mwili wa Chiume uletwe kwanza Tanzania ambako pia
ana ndugu marafiki wengi kabla ya kwenda kuzika Malawi, jambo hilo
limeshindikana.
Imeamuliwa kwamba mwili
wa Chiume upelekwe moja kwa moja Malawi ambako atazikwa Jumamosi wiki hii.
Kimwili ameondoka
duniani, lakini atakumbukwa daima kama mtu aliyechangia kufanikisha uhuru wa
Malawi na aliyeulilia umoja wa Afrika wakati wote wa uhai wake.
CHANZO: Raia mwema toleo
28 Nov 2007
No comments:
Post a Comment