HABASH: TAA YA WAPALESTINA ILIYOZIMIKA
·
Afa akiangalia mapambano ya Gaza kwenye televisheni
KWA miaka zaidi ya 41 Dk.
George Habash amekuwa nguzo ya mapambano ya Wapalestina. Kwa maana hiyo, kifo
chake, kilichotokea mwishoni mwa wiki, kimeacha pengo jingine kubwa kwa
Wapalestina; na bila shaka kiasi fulani cha ahueni kwa Israel.
Kwa mujibu wa maelezo ya
mkewe, Hilda Habash, mpambanaji huyo wa Palestina alifariki mjini Amman wakati
akiangalia taarifa ya habari ya televisheni iliyokuwa ikionyesha mapambano
yanayoendelea hivi sasa Ukanda wa Gaza.
“Wakati wa kipindi cha
kuugua kwake madaktari walikuwa wakimwambia kuwa maumivu na mateso yake ni sawa
na maumivu na mateso wanayoyapata wakazi wa Gaza hivi sasa ambako umwagaji damu
umepamba moto,” alisema Hilda.
Dk.George Habash au Dk.
GH, kama wapiganaji wengi wa Kipalestina walivyozoea kumwita, ndiye
aliyeanzisha chama cha ukombozi wa Palestina cha Popular Front for the
Liberation of Palestine (PFLP) mwaka 1967. PFLP ni moja ya vikundi vingi vya
Kipalestina vilivyokuwa vikiipa sana tabu Israel katika miaka ya 70 na 80.
Kwa miaka mingi tu PFLP
kilikuwa na ushawishi na mvuto mkubwa ndani ya Chama cha Ukombozi wa Palestina
cha PLO. Ni chama ambacho kilitumia kila aina ya mbinu, ukiwemo ugaidi,
kuhakikisha agenda ya Palestina inasikilizwa na dunia nzima.
Mara kadhaa kiliandaa na
kutekeleza mipango ya utekaji ndege za abiria za Israel au zile za nchi zenye
mahusiano na Israel, jambo lililokifanya kiogopwe na kuheshimiwa sawa na kile
cha Fatah kilichokuwa kikiongozwa na Yasser Arafat ambaye sasa naye ni
marehemu.
George Habash alizaliwa
mwaka 1926 katika familia ya Kikristo ya Lydda (Sehemu ya Israel ambayo sasa
inafahamika kwa jina la Lod). Mwaka 1948 familia hiyo ililazimika kukimbilia
Beirut baada ya taifa la Israel kuanzishwa.
Ni katika Beirut ambako
George Habash alivutiwa na fani ya tiba na hivyo kujiunga na Chuo Kikuu cha
Marekani cha Beirut – American University of Beirut, kusomea udaktari wa tiba.
Lakini ukiachilia mbali
mapenzi yake mapya katika fani ya tiba, siasa ndiyo iliyokuwa kivutio chake
kikubwa tangu akiwa mtoto. Tangu yu kijana mdogo, alipenda kujitangaza kwamba
yeye ni mwanamapinduzi wa Kiarabu. Haikushangaza, hivyo basi, alipojiunga
baadaye na kikundi kilichoitwa “Youth of Vengeance” ambacho kilihamasisha
Waarabu kuwashambulia viongozi wa serikali za Kiarabu waliokuwa na msimamo laini
dhidi ya Israel.
Akiwa amehamasishwa na
juhudi za kuwaunganisha Waarabu zilizokuwa zikifanywa na Rais wa zamani wa
Misri, Gamal Abdel Nasser, George Habash, kwa miaka mingi, alijenga imani
kwamba ni muungano wa nchi za Kiarabu tu unaoweza kuikomboa Palestina kutoka
kwa udhalimu wa Wayahudi.
Lakini baada ya ushindi mkubwa wa Israel wa mwaka 1967 katika
vita ile ya siku sita dhidi ya majeshi ya Misri, Syria na Jordan, imani hiyo ya
George Habash kwamba Umoja wa Waarabu (Pan-Arabism) ndiyo
ungeikomboa Palestina, ilianza kufifia na mwishowe kutoweka.
Hali hiyo na ukweli
kwamba alikuwa haelewani na Arafat, ilimchochea kuanzisha kikundi chake
mwenyewe cha mapambano cha PFLP mwaka huo huo wa 1967.
Katika taarifa yake ya
kwanza kuitoa baada ya kuunda kikundi hicho, George Habash alitamka “lugha
pekee ambayo adui anaielewa ni ile ya mapambano ya kimapinduzi.”
Kwa hakika, George Habash
alikuwa hatanii kwani mwaka mmoja baadaye, Julai 1968, PFLP kiliandaa na
kutekeleza mpango wa kuiteka nyara ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la
Israel la El Al. Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Rome kwenda Tel Aviv.
Tukio hilo lililozua
hisia tofauti sehemu mbalimbali duniani liliashiria kuanza rasmi kwa mbinu mpya
ya utekaji nyara katika mapambano ya Palestina dhidi ya Israel.
Kwa kiasi fulani Habash
alifanikiwa kuhakikisha suala la Palestina linakuwa kila mara katika agenda ya
dunia, lakini katika Israel na mataifa ya Ulaya wengi walimchukulia kuwa si
mwanamapinduzi wa kweli bali ni gaidi.
Mnamo Septemba 1970
Habash na wapiganaji wake wa PFLP waliteka ndege nne za mataifa ya Ulaya. Ndege
tatu kati ya hizo zililazimishwa kutua katika kiwanja kidogo cha Jordan, tukio
ambalo lilisababisha kufumuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo.
Vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe ndiyo iliyosababisha Habash na wapiganaji wake
wa PFLP kukimbia Jordan na kuhamia Lebanon.
Lakini hata pamoja na
shughuli za PFLP kuhamia Lebanon na baadaye Syria, Habash bado alihakikisha
kundi lake linakuwa na nguvu kupita vikundi vingine vyote vya Kipalestina,
ukiondoa cha Fatah cha Arafat.
Moja ya matukio makubwa
ambayo Habash atakumbukwa nayo ni lile la Mei 1972 alipofanikiwa kuvikutanisha
vikundi vitatu maarufu duniani vya kigaidi katika mkutano uliofanyika katika
kambi ya wakimbizi Lebanon. Vikundi hivyo ni Republican Army cha Ireland,
Baader Meinhof Group na Japanese Red Army.
Ni mwezi huo huo ambapo
wapiganaji wa PFLP kwa kushirikiana na wale wa Japanese Red Army walivamia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Lod wa Israel na kuua watu 26.
Miaka minne baadaye
wapiganaji wa PFLP wakishirikiana na wapiganaji wa Baader Meinhof Group
waliiteka ndege ya Air France iliyokuwa inakwenda Tel Aviv na kuilazimisha
kutua kwenye uwanja wa Entebbe nchini Uganda. Sakata hilo lilimalizika baada ya
makomandoo wa Israel kuuvamia uwanja huo na kuokoa mateka hao ambao wengi
walikuwa Wayahudi.
Kama mafahali wawili
hawawezi kukaa zizi moja, basi, ndivyo ilivyokuwa pia kwa Habash na Arafat.
Wawili hao walikuwa wakitofautiana kwa mambo mengi, na ndiyo sababu Habash
alifikia uamuzi wa kuanzisha kikundi chake mwenyewe cha PFLP.
Wakati Arafat
alipoanzisha kampeni katika nchi za Kiarabu ya kuzishawishi kukiunga mkono
Fatah badala ya PFLP, Habash alilazimika kuzigeukia nchi za Russia na China na
kuziomba zikiunge mkono kikundi chake katika mapambano dhidi ya udhalimu wa
Israel.
Uhasama kati ya wawili
hao ulizidi kuongezeka katika miaka ya tisini; hasa baada ya Arafat na kikundi
chake cha Fatah kukubali kukaa katika meza ya majadiliano na Israel, hatua
ambayo Habash aliipinga na kuiita ni ya kisaliti kwa Wapalestina.
Ni katika msingi huo huo
Habash aliyapinga vikali Makubaliano ya Oslo ambayo yalitiwa saini mwaka 1993
kati ya Yasser Arafat na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin.
Baada ya makubaliano hayo
kutiwa saini, Habash alikataa kwenda katika maeneo waliyotengewa Wapalestina
ingawa Israel ilimpa kibali cha kuingia huko kwa ajili ya mkutano ulioitishwa
mwaka 1996. Dk. Habash aliamini kwamba kama akikanyaga katika ardhi ya maeneo
hayo itatafsiriwa kuwa anayakubali na kuyaheshimu Makubaliano ya Oslo.
Lakini kiasi alivyokataa
kuyakubali Makubaliano ya Oslo na kuendelea kushikilia mtutu wa bunduki kuwa
ndiyo njia pekee ya kumaliza tatizo la Palestina, ndivyo pia chama chake cha
PFLP, kilichokuwa na mwelekeo wa Ki-Marxist, kilivyotengwa na kupungua umaarufu
duniani.
Hali hiyo ilisababisha
kufumuka kwa shinikizo ndani ya PFLP la kumtaka ajiuzulu. Shinikizo hilo
lilipoongezeka, hatimaye, Habash alifikia uamuzi wa kuachia ngazi, Aprili
2000. Hata hivyo, mpaka wakati anajiuzulu tayari PFLP kilishapokwa umaarufu na
kikundi kingine chenye msimamo mkali cha Hamas.
Baada ya kujiuzulu
uongozi, Habash aliendelea kuishi Amman ambako alifariki mwishoni mwa wiki
akiwa na umri wa miaka 82.
- CHANZO:
http://www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment