Friday, May 9, 2014

GADAFI UMOJA WA MATAIFA




Katika anga za siasa wiki hii tunayoimaliza,ilitawaliwa na viongozi wa dunia kupigana vijembe,kufanyiana dhihaka,kuonyesha hasira zao nk kupitia hotuba walizozitoa katika mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa wanasiasa hao,yawezekana kabisa kukawa hakuna mwanasiasa aliyeongelewa,kujadiliwa na kuzua mijadala mikali zaidi ya Rais wa Libya,Muammar Gaddafi kufuatia hotuba aliyoitoa katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko jijini New York. Ni kwa sababu hiyo ndio maana leo tunavuka mipaka katika ukurasa huu wa “Mwanasiasa wa Wiki” na kumweka Gaddafi.Rais wetu,Jakaya Mrisho Kikwete,naye alihudhuria kikao hicho na alihutubia.

Kwanini “Mwasiasa wa Wiki” hapa KUKUBATA awe Kanali Gaddaffi? Sababu ni nyingi.Lakini kwa uchache,Muammar Gaddafi ni mwafrika. Hivi sasa anashikilia cheo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Kwa hiyo,kwa mapana na marefu,alikuwa akituwakilisha waafrika. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mara yake ya kwanza kutembelea/kufika  Marekani.

Safari ya Gaddafi ya kuelekea New York ilikumbana na vikwazo vingi.Kwanza alikataliwa sehemu kadhaa kuweka hema lake ambalo amekuwa akisafiri nalo kila mahali anapokwenda.Huwa hafikii hotelini.Anachohitaji yeye ni sehemu ya kuwekeza hema lake.Ulinzi wake huwa ni wa ma-bodyguard wanawake
watupu.Maandamano kadhaa kutoka jumuiya mbalimbali yakipinga Gaddafi kupewa ruhusa ya kuweka hema yalifanyika.”Hatumtaki katika mji wetu wala mtaa wetu” Gaddafi ni dikteta.Mabango kadhaa yaliweka wazi sababu za kumkatalia “mgeni”Ilibidi afikie katika “ofisi” ya kidiplomasia ya Libya.
Yote tisa.Kumi ni pale alipolikwaa jukwaa la Umoja wa Mataifa na kuanza kuhutubia.Gaddafi alihutubia muda mfupi tu baada ya Rais wa Marekani,Barack Obama, ambaye naye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuhutubia baraza hilo.Gaddafi alikuwa ametengewa dakika 15 za kuhutubia.Alihutubia kwa zaidi ya dakika 90! Wengine walidhani alikuwa akielekea kuweka rekodi ya dunia.Hakuweza kwani mpaka leo mtu ambaye anashikilia rekodi ya kuhutubia Baraza la Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu zaidi ni aliyekuwa Rais wa Cuba,Fidel mwana wa Castro.Alihutubia kwa zaidi ya masaa manne(4).

Baada ya hotuba ya Gaddafi,swali kubwa lililobakia miongoni mwa wafuatiliaji wengi wa mambo ya siasa ni “What was he talking about?”. Wengi hawakumuelewa alipotaka,kwa mfano,uchunguzi wa kina ufanyike kutokana na vifo vya aliyekuwa Rais wa Marekani,John F.Keneddy na mwanaharakati maarufu Mchungaji Martin Luther King.Uchunguzi leo hii? Gaddafi alionekana kutokuwa na maandalizi ya kile alichotaka kukiongelea.Hili hata mimi nililiona.

Alipanda na vipande chungu mbovu vya makaratasi na mara kadhaa alionekana kusahau alichotaka kusema au alikiandika kwenye kipande gani cha karatasi.Mara kadhaa alijichanganya hususani alipokuwa anaongelea homa ya mafua ya nguruwe ya Swine Flu.
Pamoja na “hitilafu” hizo,yapo mambo ya msingi ambayo Kanali Muammar Gaddafi aliyaongelea.Kwa mfano ni kweli kwamba nchi nyingi wanachama wa UN hivi leo,hazikuwa wanachama wakati umoja huo unaanzishwa.Kwa hiyo,kuna haja ya kuangalia upya muundo mzima wa umoja huo yakiwemo mambo kama vile kura ya Veto.Gaddafi pia aliongelea jinsi ambavyo madhumuni ya kuanzishwa kwa umoja huo yameshindwa.Alisema,kwa mfano,vita zaidi ya 65 vimetokea na vinaendelea kutokea huku umoja huo ambao ulianzishwa ili kuzuia kutokea kwa vitu kama vita,ukiangalia tu.Ukitaka kusoma hotuba na kusikiliza hotuba nzima ya Muammar Gaddafi,bonyeza hapa.
Je ulipata muda wa kuiangalia hotuba ya Gaddafi?Unasemaje kuhusu hotuba hiyo? Gaddafi alitoa uwakilishi ulioutegemea kwa bara la Afrika? Unakubaliana na wanaosema Gaddafi ni mzigo kwa bara la Afrika na sababu nyingine ya kudharauliwa?
Viongozi wengine waliohutubia na kuzua gumzo ni Rais wa Iran,Mahmoud Ahmadenijad ,Rais wa Zimbwabwe,Comrade Robert Gabriel Mugabe na kama kawaida Rais wa Venezuela Hugo Chavez aliyeanza kwa kuomba wasikilizaji wake wasije wakamrushia kiatu ikiwa ni dongo la moja kwa moja kwa Rais wa 43 wa Marekani,George Bush iliyembidi akwepe viatu vya mwandishi wa habari wa Iraq alipokuwa madarakani.
CHANZO: kutoka katika mtandao

No comments:

Post a Comment