Mikhail Timofeyevich Kalashnikov
·
Mbunifu wa bunduki aina ya AK 47,
Mikhail Timofeyevich
Kalashnikov (94) ameaga dunia juzi lakini ameiachia dunia urithi wa silaha ya
bunduki aina ya AK 47 Kalashnikov; silaha inayoelezwa kuua watu wengi duniani
kuliko nyingine yoyote.
Kalashnikov, aliyegundua
silaha hiyo wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, alifariki dunia kijijini kwake
Izhevsk, baada ya kuugua kwa takribani mwezi mmoja kutokana na magonjwa
mbalimbali yaliyosababishwa hasa na umri wake mkubwa.
Askari huyu wa aina yake
katika karne iliyopita, aligundua silaha hii wakati alipokuwa akifanya kazi
katika Jeshi la Urusi wakati huo na akiwa na umri wa miaka 22 tu.
Watu wengi wanadhani AK
47 iligunduliwa kwa kazi ya siku moja, lakini ukweli ni kwamba kazi ya
kutengeneza na hatimaye kuimaliza silaha hii ilichukua muda wa takribani miaka
sita ya majaribio.
Katika mahojiano
aliyofanyiwa miaka minne iliyopita wakati alipokuwa akifanyiwa sherehe rasmi ya
kutimiza miaka 90, Kalashnikov alisema hajutii kwamba silaha aliyobuni imeua
watu wengi namna hiyo.
“Wakati nikitengeneza
silaha hiyo, lengo langu halikuwa kuua mtu bali kulinda taifa langu. Kama
baadaye imeanza kutumiwa na magaidi kuua watu, hilo halikuwa lengo langu.
“Hata hivyo, kusema
ukweli ningefurahi zaidi kama ningeweza kubuni kifaa ambacho kingetumiwa na
wakulima kwa namna ile ile ambayo AK 47 imetumika duniani kote. Pengine kwa
namna hiyo ningeisaidia zaidi dunia,” alisema.
Hii ni silaha ambayo
inapatikana karibu kote duniani. Kuna maeneo barani Afrika ambako watoto wa
kiume wanaozaliwa huitwa Kalash kwa heshima ya silaha hiyo.
Katika baadhi ya bendera
za taifa, silaha hii inaonekana. Nchi kama Zimbabwe na Burkina Fasso ni mfano
wa nchi zilizoamua kabisa kuweka silaha hii kama mojawapo ya alama za taifa.
Katika soko la silaha
leo, Kalashnikov (AK47) inaweza kupatikana nchini Afghanistan kwa thamani ya
pauni tatu za Uingereza (shilingi elfu sita za Tanzania) na nchini India,
silaha hiyo hiyo inaweza kupatikana kwa bei ya pauni 3,000 (shilingi milioni
sita).
Kwa ujumla, rekodi
zilizopo zinaonyesha kwamba kuna bunduki zaidi ya milioni 100 za aina ya AK 47
duniani kote. Kwa nini 47 zimekuwa maarufu sana?
Bunduki hizi ni mongoni
mwa bunduki chache zilizopo duniani ambapo unaweza ukazizamisha kwenye maji na
bado ikafyatua risasi kama kawaida.
Kalashnikov inaweza pia
kufanya kazi katika mazingira yoyote. Iwe kwenye baridi kali kama ya Russia au
joto kali kama la nchi zilizo jirani na ukanda wa Ikweta, AK 47 inafanya kazi
zake bila ya matatizo.
Pia, silaha hii
imejijengea sifa ya kuwa rahisi kujifunza kwani watu wanaoifahamu vizuri silaha
hii wanasema mtu anaweza kufundishwa kuitumia katika muda wa saa nzima na akawa
anaweza kuitumia.
Sifa nyingine iliyoipa
umaarufu mkubwa silaha hii ni ile ya kuweza kusafishika kwa muda mfupi kuliko
silaha nyingi zilizopo sasa na hii maana ya hii ni kwamba, haihitaji gharama
kubwa kuifanyia matengenezo.
Umaarufu wa mgunduzi
Katika mahojiano
aliyowahi kufanyiwa na jarida la Telegraph la Uingereza miaka kumi iliyopita,
Kalashnikov alitoboa siri ya kwa nini ilimchukua muda mrefu kufahamika nje ya
taifa lake ingawa silaha aliyoibuni ilikuwa maarufu nje ya Urusi.
“Kabla ya mwaka 1990,
mimi nilifanywa siri na taifa langu. Sikuruhusiwa kusafiri nje ya Urusi kwa
sababu yoyote ile bila ya serikali kufahamu. Inaonekana serikali ilihofu kwamba
naweza kuibwa na uwezo wangu kutumikia mataifa mengine.
“Ni mpaka baada ya mwaka
1990 ndipo hasa nilipoanza kutoka nje ya Russia kwa kutumia jina langu halisi.
Kabla ya hapo, hata niliposafiri nje ya nchi, nilikuwa nikitumia jina la
bandia,” alisema.
Ni katika mahojiano hayo
ndipo mgunduzi huyu alipowashangaza Waingereza kwa kuwaambia kwamba kwa maoni
yake AK 47 si silaha bora kuliko zote zilizowahi kutengenezwa na kuwa ana imani
ya kuwa ipo siku, itakuja silaha nyingine kubwa kuliko hiyo.
Kuna habari moja ya mzaha
kati ya Kalashnikov na mgunduzi mwingine maarufu wa silaha katika Jeshi la
Marekani, Eugene Stoner, aliyetengeneza bunduki aina ya M16. Kuna wakati
walikutana nchini Marekani na kila mmoja akaanza kusifia ubora wa silaha yake.
Stoner alisema uzuri wa
AK 47 unatokana na ukweli kwamba unabeba risasi nzito zaidi na hivyo uwezekano
wa kuwa na shabaha ni mzuri kuliko Kalashnikov, lakini Mrusi huyo akajibu
kwamba silaha nyepesi ni nzuri kwa sababu ni rahisi kubebwa.
Ubishi huo ulimalizwa
katikati na mmoja wa makamanda wa majeshi ya Marekani ambaye alipomwona
Kalashnikov, alimwambia; “Niliikumbuka sana bunduki yako wakati wa Vita ya Vietnam.
Kama tungekuwa na AK 47 za kutosha, huenda vita ile ingekuwa na matokeo
tofauti.” Maneno hayo murua ya Jenerali huyo wa Marekani yalimaliza
ubishi huo wa Stoner na Mikhail.
“Kusema kweli, sisi
wagunduzi wa bunduki hatukuwa na nia mbaya hata kidogo. Ukiangalia kwa undani
utaona kwamba lengo letu la kwanza lilikuwa ni kupambana na ufashisti.
“Lakini yaliyokuja
baadaye ni maafa. Bunduki aliyoitengeneza Stoner ilitumika kuua raia wa Vietnam
waliokuwa wakitetea uhuru wa taifa lao. Maafa makubwa. Bunduki iliyobuniwa na
Uziel Gal (Uzi) imetumiwa sana kuua Wapalestina na jirani zao.
“Mimi nashukuru kwamba
bunduki yangu niliyoibuni kuna watu wameifurahia. Sitasahau tukio moja
lilitokea nchini Msumbiji ambapo viongozi wa serikali hiyo walinipa mwaliko kwa
kusema; Kalashnikov, karibu nchini kwetu kwani bunduki yako ndiyo imetupa
uhuru.
Wapo askari ambao wamewapa jina la Kalash watoto wao wa kwanza wa kiume
waliozaliwa baada ya ukombozi kwa sababu ya silaha hiyo,” alisema.
Kalashnikov na kubadili
dini
Wakati mmoja, Kalashnikov
alikuwa ametembelea nchini Saudi Arabia na alikuwa katika Uwanja wa Ndege wa
Riyadh wakati mmoja na wenyeji wake alipozungumza neno ambalo limekuwa
likirudiwa mara kwa mara.
“Mikhail, kwa nini
usiamue tu kubadili dini kutoka Ukristo na kuwa Muislamu? Kwenye dini ya
Kikristo, wewe unachukuliwa kama mtu uliyeua watu wengi na mdhambi.
“Lakini sisi katika dunia
ya Uislamu, huku Mashariki ya Kati, jina lako linavuma. Hata bendera ya kundi
linalochukuliwa kuwa la kigaidi la Hezbollah limeweka AK 47 kwenye bendera
yake,” aliambiwa na mwenyeji wake huyo.
Kalashnikov alikataa ofa
hiyo ya aina yake kwa upole. Kuna msemo katika ngano za kale za Urusi kwamba
kubadili imani ya mtu ni kitu kigumu kwani imani si shati la kuvaa ambalo mtu
anaweza kulibadili wakati wowote.
Amefaidika vipi na
ubunifu wake?
Kutokana na majaribio
aliyokuwa akifanya mara kwa mara ya bunduki zake, Kalashnikov alimalizia maisha
yake ya uzeeni akiwa na nusu kiziwi. Ili kuzungumza na mgunduzi huyu, ilimpasa
mtu kuzungumza naye akiwa jirani na sikio lake.
Na madhara haya hayakuwa
kwake pekee. Wapo watu wengine ambao walikuwa wakiishi jirani naye kule
kijijini kwake Izhev walioathirika na majaribio yake ya silaha ya mara kwa
mara.
Kama mbunifu huyu
angekuwa amezaliwa Marekani, leo angekuwa mmoja wa matajiri wakubwa lakini kwa
sababu hakuweza kuiwekea silaha yake hiyo hatimiliki kwa sababu ya nchi yake
kufuata sera za ukomunisti, amekufa akiwa mstaafu wa kawaida wa jeshi.
Mikhail alijiunga na
Jeshi la Urusi miezi akiwa na umri wa miaka 19 tu. Yeye alikuwa mtoto wa
mkulima tajiri ambaye hakupendwa na sera za ukomunisti na hatimaye yeye na
familia yake wakafukuzwa kwao na kwenda kuishi Siberia.
Enzi ya utawala wa
Kikomunisti wa Vladmir Lenin, familia yoyote iliyohamishiwa Siberia ilikuwa ni
sehemu ya adhabu.
Walipokuwa Siberia ndipo
kipaji cha ugunduzi cha Kalash kilipoanza kujulikana. Kwa sababu hakukuwa na
mashine ya kusaga, kijana huyu mdogo alibuni mashine maalumu ya kusaga ambayo
baadaye ilikuja kutumika kusagia mtama na ngano iliyokuwa ikitumiwa na wananchi
wenzake.
“Shida na mateso ambayo
familia yangu ilikuwa ikiyapata ndiyo yaliyonifanya nikawa mpambanaji wa
kiwango cha juu. Nikajua, kama nisipokuwa mbunifu, kuna hatari ya familia yangu
na mimi binafsi kuteketea,”alisema.
Hata hivyo, Kalashnikov
anaamini kwamba alizaliwa na kipaji cha ugunduzi kwani tangu angali mdogo, siku
zote alikuwa akibuni vitu adimu.
“Unajua ugunduzi ni sawa
na kuwa mama mwenye mtoto tumboni. Ni lazima umchunge mwanao na uhakikishe
anazaliwa akiwa salama. Unajua kosa lako moja tu linaweza kusababisha madhara
kwa mtoto.
“Kama ugunduzi wako
utauchukulia kwa umakini ule ule ambao mama mjamzito na anayelea mtoto mdogo
anakuwa nao, uwezekano wa kuwa mgunduzi mzuri nao unaongezeka,” alipata kusema
Kalashnikov.
Kuna wanaosema kwamba
endapo Kalashnikov angezaliwa Marekani, huenda angevumbua silaha nyingi zaidi
kutokana na namna teknolojia ilivyokua sana na uhuru uliopo pamoja na
uwezeshaji ambao wagunduzi wanapewa wakiwa nchini humo.
Baadaye Mikhail aliamua
kujiunga na Jeshi la Urusi ambako alijiunga katika kikosi cha Mizinga lakini
wakati tayari akiwa ameanza kuonyesha uwezo wake kwenye eneo hilo, alipata
shambulio lililoathiri bega lake na hivyo kutofaa tena.
Ni katika kipindi alipokuwa
hospitali akiuguza jeraha lake hilo, ndipo Kalashnikov alipoanza kupata picha
ya aina ya silaha anayotaka kuitengeneza. Silaha nyepesi kuibeba, inayoweza
kumudu mazingira magumu, rahisi kutumia na yenye shabaha nzuri.
Ndipo hapo ilipozaliwa AK
47.
Kabla hajaibuni AK 47,
zilipita aina nyingine tofauti za bunduki kama vile STi 444 ambayo ilitumika
kidogo lakini haikuwa na umahiri wa kutosha lakini yenyewe ndiyo iliyofungua
njia kwa Kalashnikov.
Majigambo ya AK 47
Baadhi ya viongozi
wamekuwa wakiitumia silaha hii kuonyesha majigambo yao. Katika enzi alizokuwa
Rais mwenye nguvu wa Irak, Saddam Hussein al Tikrit, alikuwa akipenda kufyatua
bunduki yake aina ya AK 47 hadharani kwenye mikutano ya hadhara.
Mwenyewe alikuwa akipenda
kufyatua risasi hewani huku akiwa ameishikilia bunduki yake kwa mkono mmoja.
Katika picha mbalimbali
za televishenia alizokuwa akipiga na kutoa matamshi yake mbalimbali dhidi ya
Marekani na vibaraka wake, Osama bin Laden , mara zote alikuwa akionekana huku
akiwa na AK 47 yake pembeni.
Na hili sasa limeigwa pia
na aliyekuwa namba mbili wake, Ayman al Zawahri.
Shujaa au Gaidi?
Wakati safari ya Mikhail
Kalashnikov kwenda kaburini ikiwa imeiva, dunia imegawanyika kuhusu namna
ya kumkumbuka mtu kama yeye. Wanaojiita wapenda amani wanawalaumu watengeneza
silaha kwa kuisababishia dunia maafa kwa kutengeneza vitu vinavyosababisha watu
wasitake kukaa chini na kuzungumza.
Lakini, ukizungumza na
wapigania uhuru kama wa Msumbiji na katika nchi za kiarabu, AK 47 inahusishwa
na ukombozi wao. Wapo wanaomini kwamba bila ya silaha hiyo, huenda wangedumu
kwenye ukoloni kwa muda mrefu.
Kama dunia ingekuwa haina
silaha hata moja, huenda ingekuwa sehemu ya amani na utulivu. Lakini, wana
saikolojia wanasema isingewezekana kwa dunia kuishi bila ya silaha kwa sababu
mwanadamu kwa asili ni mbinafsi na angetafuta namna yoyote ya kushinda kwenye
ushindani.
Pengine watu kama
Kalashnikov ni sehemu ya ubinadamu wetu. Kama watu kama wao wasingekuwepo,
labda dunia isingekuwa sehemu nzuri ya kuishi kuliko ilivyo sasa.
CHANZO:mikhail-timofeyevich-kalashnikov#sthash.Nwtg9GKp.dpuf
No comments:
Post a Comment