Jonas Malheiro Savimbi
alizaliwa Agosti 3, 1934 katika mji wa Munhango, Jimbo la Moxico katika
kitongoji cha Reli ya Benguela, nchini Angola.
Savimbi, alikuwa
mwanasiasa na mwanzilishi wa Chama cha Unita, ambaye pia alikuwa kiongozi wa
Jeshi la Ukombozi la Unita, kama ambavyo mwenyewe alikuwa akiliita.
Baba yake Savimbi
alikuwa Mkuu wa Kituo cha Reli Benguela enzi za ukoloni na pia mchungaji wa
Kanisa la Kiprotestant lilioanzishwa na Misionari kutoka Marekani.
Awali, kundi la waasi
wa Unita lilianza kama kundi la wapiganaji wa msituni waliokuwa wakipambana na
utawala wa kikoloni wa Ureno kuanzia mwaka 1966 mpaka mwaka 1974.
Baada ya kupatikana
uhuru mwaka 1975, Savimbi na kundi lake waligeuka na kuwa kundi la waasi na
kuanzisha vita dhidi ya Serikali ya Chama cha MPLA.
Uasi huo ulizaa vita
ya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1975 mpaka mpaka Februari 22 mwaka 2002.
Vita ilikomaa baada ya Savimbi kuuawa na wanajeshi wa Angola.
Savimbi alikuwa
kiongozi pekee wa waasi wa msituni
waliopigana ndani ya Angola mpaka taifa hilo
lilipopata uhuru.
Mwaka 1991, Unita
ilikubali kusaini mkataba wa kusitisha mapigano na MPLA na kukubaliana kuwa
chama hicho cha Savimbi kiwe huru kushiriki chaguzi mbalimbali.
Hata hivyo, pamoja na
kushiriki chaguzi hizo, Unita ilishindwa kupata ushindi mwaka 1992, jambo
lililomchukiza Savimbi na kuamua kurudi msituni kupambana na Serikali ya
Angola.
Inadaiwa kuwa Savimbi
alikuwa akipata msaada wa kijeshi kutoka nchi za Afrika Kusini, China na Marekani,
wakati Serikali ya Angola ilikuwa ikipata msaada kutoka Urusi.
Savimbi aliyelelewa
kwenye mazingira ya Kikristu na kusoma shule za seminari za Kiprotestant na
Katoliki, anadaiwa kunusurika majaribio 15 ya kuuawa kutoka kwa wanajeshi wa
Angola.
Hata hivyo, mwisho wa Savimbi ulikuwa Februari
22, 2002 alipovamiwa kwenye ngome yake ya kijeshi kwenye mji alikozaliwa na
kuuawa na majeshi ya Angola, yaliyokuwa yakimsaka kwa muda mrefu.
Taarifa za kuuawa
Savimbi zilipokelewa kwa shangwe nchini Angola kutokana kuonekana kama kiini
cha kukosekana kwa amani nchini huko na majirani zake.
Kituo cha Televisheni
cha Serikali kilionyesha picha ya Savimbi akiwa amelazwa chini bila nguo, huku
akiwa na matundu 15 ya risasi sehemu mbalimbali mwilini na nyingi kichwani.
Kuna taarifa zinadai
kuwa, Savimbi alikamatwa akiwa hai kutokana na majeraha aliyopata wakati wa
mapambano, na aliuawa baada ya kuteswa kwani alipigwa risasi kwenye miguu na
mikono yote, shingoni na kifuani.
Baada ya kuuawa
Savimbi, nafasi yake ilichukuliwa na Antonio Dembo, ambaye alijeruhiwa katika
shambulizi lililomuua Savimbi na siku 10 baadaye alifariki dunia. Wiki sita
baada ya kuuawa Savimbi, mkataba wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya
UNITA na MPLA ulisainiwa, huku ikiiacha Angola kugawanyika kisiasa katika
makundi mawili, MPLA na UNITA.
Savimbi anakumbukwa
kwa ukatili mkubwa aliolekeza majeshi yake kufanya dhidi ya majeshi ya Angola
katika vita iliyodumu kwa miaka 26 kabla ya kumalizika.
Mara kadhaa alikuwa
akiwataka askari wake kuwaua kikatili askari wa Jeshi la Angola kwenye uwanja
wa mapambano. Hakutaka mateka, aliamuru wauawe kukatwa vichwa au kufa kwa
kupewa mateso makali.
CHANZO: kutoka katika vyanzo mbalimbali katika mtandao.
No comments:
Post a Comment