Tuesday, January 28, 2014

LIBYA BAADA YA KIFO CHA GADDAFI








miaka  chache baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, walibya na dunia kwa ujumla imeingia katika mitizamo tofauti kuhusu kiongozi huyo huku wengi wakikumbuka mafanikio aliyoleta kwa taifa 


hilo tofauti na viongozi wengine waliong’olewa kwa udikteta.Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikimtangaza na kutafuta namna zote za kujenga picha ya udikteta bila kuangalia upande wa pili wa Libya iliyooachwa na Gaddafi.


Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumziwa ni iwapo Libya ya sasa itaweza kuneemeka na kile ambacho ilikuwa ikipata kutoka kwa kiongozi huyo, ambaye hivi karibuni aliuawa na wapinzani wake.


Gaddafi, tofauti na viongozi wengine waliowahi kutajwa kuwa madikteta duniani, ana mengi ya kukumbukwa na kusifiwa kwayo.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuongozi wamekuwa wakieleza kusikitishwa kwao na kutotambua aina ya demokrasia ambayo baadhi ya watu wa Libya wanaililia kwa sasa na iwapo itaboresha au kuharibu kabisa maisha yao.


Hii inawekwa wazi kwamba pamoja na kwamba Gaddafi ametumia fedha nyingi za Libya katika masuala binafsi, lakini je, kwa wastani Libya ni maskini? Wapo viongozi waliozitumia nchi zao na kuziharibu kabisa, Gaddafi aliwahi kuifilisi Libya?


Haya ni baadhi ya mambo ambayo Gaddafi aliyasimamia na kuyatekeleza katika utawala wake wa miaka 42 kwa Libya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na tovuti za mawasiliano za Libya na Zimbabwe zimeeleza kuwa nchini Libya hakuna mwananchi aliyewahi kulipa bili ya umeme, umeme ulikuwa bure kwa raia wake wote.


Hakukuwa na riba katika mikopo, benki zote Libya zilikuwa chini ya Serikali, mikopo ilitolewa kwa wananchi bila riba ya kiasi chochote .


Taarifa hizo zikafafanua kuwa makazi ni haki ya msingi nchini Libya, Gaddafi aliwahi kusisitiza kwamba wazazi wake hawawezi kupata makazi hadi kila raia apate makazi. Baba wa Gaddafi alifariki dunia wakati yeye, mama yake wakiwa wanaishi katika hema.


Wanandoa wote wapya nchini humo walipata Dola 50,000 kwa Serikali kwa ajili ya kununua makazi yao kuwasaidia kuanzisha familia mpya.
Elimu na huduma za kiafya vilitolewa bure. Wakati Gaddafi nachukua nchi asilimia ya waliokuwa na elimu ilikuwa 25, kwa sasa inafikia 83.


Kwa waliotaka kuwa wakulima, walipewa ardhi bure, nyumba katika shamba lao, vifaa, mbegu na mifugo kwa ajili ya kuanzisha miradi.
Iwapo kuna waliokuwa hawawezi kupata huduma za elimu na afya wanazostahili, Serikali iliwalipia kwa ajili ya kuzipata nje ya nchi, hizi hazikuwa bure, walitakiwa kuchangia, walipata Dola2,300 kwa mwezi kwa ajili ya makazi na usafiri.


Kwa waliokuwa wakitaka kununua magari, Serikali ililipia kwa asilimia 50 ya bei. Bei ya petroli ilikuwa karibu na bure, lita ililipiwa kwa Dola 0.4.


Libya haidaiwi nje, pia ina akiba inayofikia Dola150 bilioni nje ambayo kwa sasa imezuiliwa.Kwa waliomaliza vyuo, Serikali iliwapatia posho sawa na mshahara wa maofisa hadi watakapopata ajira yenye uhakika.
Sehemu ya mauzo ya mafuta ya Libya iliwekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya raia wake.


Kila mwanamke aliyejifungua alipata posho ya Dola5000, mikate 40 iliuzwa kwa dola0.15, asilimia 25 wa Walibya, wana shahada ya chuo kikuu.
Kama hiyo haitoshi taarifa hizo zimeeleza kuwa alisimamia mradi mkubwa kabisa wa umwagiliaji, uliopewa jina la Great Man-made River, kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye maeneo yote ya nchi yenye jangwa.


Wakati wa vikwazo kwa Serikali yake miaka ya 1980, Libya ilikuwa miongoni mwa nchi tajiri kabisa kwa msingi wa pato la ndani, ikwa na kiwango cha juu cha maisha kuliko Japan.
Ilikuwa ni nchi tajiri kuliko zote kabla ya vuguvugu la mapinduzi.

Wastani wa kiwango cha maisha kwa pato la kichwa ni Dola11,314
. Gaddafi amewahi kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari zake na miradi yake, lakini amefanya mabo makubwa ambayo hakuna dikteta aliyewahi kuyafanya kwa watu wake. Alirejesha pato kwa watu wake, aliwajali.


Wosia wa Gaddafi kabla ya kifo 
Katika wosia wake, Kanali Gaddafi aliwaasa wafuasi wanaomuunga mkono kuendelea kupambana.

Alielezea msimamo wake kuwa amechagua kupambana hadi hatua ya mwisho na kufia katika ardhi ya Libya kuliko kuchagua njia nyepesi, ambayo kwa mtizamo wake, ni kitendo cha kujidhalilisha kisichokuwa na heshima, kukimbilia uhamishoni nje ya nchi yake, ambapo tayari alishapata ahadi nyingi za ulinzi.


Katika lugha ya Kiingereza, waraka wake wa wosia umetafsiriwa ukisomeka: “Hii ni hiyari yangu. Mimi Muammar bin Mohammad bin Abdussalam bin Humayd bin Abu Manyar bin Humayd bin Nayil al Fuhsi Gaddafi, ninaapa kwamba hakuna Mungu mwingine zaidi ya Allah na Muhammad ni Mtume wake, amani iko kwake. Ninaahidi nitakufa nikiwa Muislamu.


“Iwapo nitauawa, nitapenda kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za kiislamu, nikiwa nimevaa mavazi nitakayokuwa nimevaa wakati kifo change kikitokea, bila mwili wangu kuoshwa, katika makaburi ya Sirte, jirani na familia na jamaa zangu.


“Nitapenda kwamba familia yangu, hasa wanawake na watoto, watunzwe vyema baada ya kifo changu.

Watu wa Libya wana wajibu wa kulinda wasifu, mafanikio, historia na heshima ya waasisi na mashujaa wake.


“Watu wa Libya hawatakiwi kupuuza kujitapa na lazima wawe watu huru wa kuthaminiwa.
Ninawataka wale wanaoniunga mkono kuendelea kupambana, kuwakabili wote wanaosimama kutoka nje dhidi ya Libya, leo, kesho na siku zote.


“Hata kama hatutashinda mapema, tutatoa funzo kwa vizazi vyetu vijavyo, kwamba kuchagua kulinda utaifa ni heshima na kuliuza ni uasi mkubwa ambao historia haitausahau milele, pamoja na juhudi za wengine kuwaeleza kinyume cha hayo”.



Msimamo wa Serikali ya Mpito ya Libya
Mustafa Abdul Jalil Kiongozi wa Baraza la Mpito la Libya alisema juzi kwamba sheria za Kiislamu zitakuwa msingi muhimu wa utungaji sheria nchini Libya.


Akizungumza katika mji wa Benghazi katika sherehe za kutangaza kukombolewa kwa nchi hiyo kutoka mikononi mwa utawala wa Gaddafi,
Abdul Jalil alisema kuwa Libya ikiwa ni nchi ya Kiislamu itatunga sheria zake kutokana na mafundisho ya Kiislamu na kwa msingi huo sheria zote zilizokuwa zikitumiwa na utawala wa Gaddafi kupiga vita Uislamu zitafutwa.


Alizishukuru Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kwa kuisaidia Libya kumwondoa madarakani Gaddafi.


Abdul Jalil pia alizungumzia mipango ya kuanzisha Benki za Kiislamu nchini Libya hivi karibuni na kuongeza kuwa benki hizo hazitakuwa zikichukua wala kutoa riba na kwamba zitatekeleza shughuli zao kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu.

Alisema kwamba mapinduzi ya wananchi wa Libya yalianza kwa amani, lakini yalikabiliwa na vitendo vya mabavu na nguvu kutoka kwa utawala wa dikteta Gaddafi.

MISRATA, Libya
MWILI wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Maummar Gaddafi umezikwa katika sehemu ya siri jana, baada ya kuuawa kwake na wapiganaji waliokuwa wakimpinga wiki iliyopita.



Mmoja wa waopiganaji hao alijitokeza kwa mara ya kwanza jana kupitia mkanda wa video akieleza kwamba yeye ndiye aliyechukua uamuzi wa kufyatua risasi na kumuua Gaddafi, kwa kuwa hakuona haja ya kumshikilia akiwa hai.


Maziko hayo yamefanyika baada ya kuwapo kwa mvutano baina ya wanafamilia wa Kanali Gaddafi na uongozi wa sasa wa Libya ambao ni Baraza la Mpito la Nchi hiyo (NTC) ambalo lilitangaza kuzika mwili huo kwa siri, ili kuficha mahali lilipo kaburi la kiongozi huyo wa Libya kwa miaka 42.


Mwili huo ulichukuliwa na kupelekwa kuzikwa kusikojulikana, baada ya ndugu na watu wake kadhaa wa karibu kuruhusiwa kushiriki katika sala maalum na taratibu zote za Kiislamu.


Mmoja wa wasemaji wa NTC alisema jana kuwa mwili wa Gaddafi, mwanae Mutassim pamoja na mmoja wa wasaidizi wake imezikwa, licha ya kuwapo kwa utata kuhusu pale ilipostahili kuzikwa.


Mvutano uliokuwapo ulitokana na ombi la ndugu wa kabila la Kanali Gaddafi ambao walikuwa wakitaka wapewe mwili wa kiongozi huyo ili wauzike mjini Sirte, alipozaliwa, lakini viongozi wa baraza la kitaifa la mpito walipinga ombi hilo.


Taarifa nyingine zinamnukuu msemaji wa NTC, Ibrahim Beitalmal akisema ndugu wachache wa familia ya Gaddafi walishiriki katika taratibu za ibada ya mazishi ya kiongozi huyo na dua, vilivyofanyika kwa kuzingatia taratibu za dini ya Kiislamu.


Hata hivyo, habari zaidi zinadai kuwa, baada ya sala hiyo, ndugu wa Gaddafi hawakuruhusiwa kuona sehemu ambayo kiongozi huyo amezikwa ambako kunadaiwa kuwa ni katikati ya jangwa.


Baadhi ya watu mjini Misrata wanasema miili ya watu hao watatu iliondolewa usiku kutoka sehemu ilipokiuwa imehifadhiwa katika harakati za kupanga mazishi hayo.


Raia wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la bucha katika mji wa Misrata ambako miili hiyo ilipelekwa na kuhifadhiwa baada ya tangazo la kifo cha kiongozi huyo na baadhi ya walinzi wake, kujionea mwili wake ili kuthibitisha ukweli kuwa ameuawa.


Viongozi wa NTC walikuwa wanahofia kuwa huenda Kanali Gaddafi akizikwa katika sehemu ya wazi, kaburi lake litabadilishwa kuwa pahali patakatifu na wafuasi wake.


Pamoja na hilo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza uchunguzi ufanyike kubainisha jinsi alivyouawa Kanali Gaddafi, kwani picha za awali zilionyesha kuwa alikamatwa akiwa hai.


Kiongozi wa NTC, Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuwa uchunguzi utafanyika kuhusu hilo. Hata hivyo, kuna wale wanaohoji ikiwa kweli uchunguzi huo utakuwa wa wazi ikiwa mashirika ya kujitegemea hayakuhusishwa.

Katika video iliyotolewa jana, kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kijana mpiganaji anayedai kumuua Kanali Gaddafi baada ya kukamatwa akiwa hai kwenye mtaro wa majitaka, alisema hakuona sababu ya kumuacha aendelee kuwa hai na kumkabidhi kwa uongozi wa NTC.

“Tulimkamata, nilimpiga katika paji la uso. Baadhi ya wapiganaji wenzangu walikuwa wakilazimisha kutaka tumpeleke na kumkabidhi akiwa hai. Niliamua kumpiga risasi mbili. Moja kichwani na nyingine kifuani,” alisema.

Katika kutaka kuthibitisha hilo, kijana huyo alionyesha kipande cha nguo ya Gaddafi kikiwa kimetapakaa damu na pete ya dhahabu ambayo alimvua baada ya kumuua.

MISRATA, Libya
ALIYEKUWA kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alitoa ahadi ya utajiri wa fedha na dhahabu kwa watu waliomtia nguvuni, ikiwa ni katika kujaribu kuokoa uhai wake.

Mmoja wa mashuhuda, Hammad Mufti Ali (28) alieleza namna kiongozi huyo alivyowaahidi utajiri tofauti vijana waliobaini maficho yake kwenye mtaro wakupitisha maji barabarani jambo ambalo lilikuwa ni tofauti na matarajio yao.

Ushuhuda huo umetolewa huku kukiwa na utata kuhusu nini kilichotokea katika dakika za mwisho za kifo cha Kanali Gaddafi, ambaye mazishi yake yameendelea kucheleweshwa kutokana na wito wa kutaka kufanyika kwa uchunguzi.

Ali ambaye ni kamanda wa brigedi moja ya kijeshi katika Mjini wa Sirte, alikaririwa na Gazeti la Coriette Della Sera la Italia akisema baada ya kutolewa katika mtaro, kisha kusukumwa huku na kule, alitoa ahadi nyingi akiomba asiuawe.

“Alisema yuko tayari kutoa chochote ili kulinda uhai wake. Alisema anazo fedha na dhahabu kwa ajili yetu iwapo tutamwacha akiwa hai.”

“Alikuwa akitokwa na damu nyingi, alikuwa na umri wa miaka 69 hivyo mwili wake usingeweza kuhimili. Alikuwa katika hali mbaya sana. Alikuwa na majeraha kila sehemu ya mwili wake, ya risasi na yaliyotokana na kipigo,” alisema na kuongeza:

“Kuna wakati mmoja wetu alipayuka akimwambia kuwa badala ya kuzungumza kuhusu fedha, kama Mwislamu mwadilifu, anatakiwa kuomba kwa ajili ya nafsi yake iweze kupokewa mbinguni kabla hajafa. Lakini aliendelea kusisitiza kwamba yuko tayari kutupa fedha nyingi na dhahabu nyingi kadiri iwezekanavyo”.

Kanali Gaddafi alionekana akitolewa katika mtaro huo wa maji wa barabarani akiwa hai, huku akiwa na majeraha kadhaa ya risasi.

NTC yajikosha

Hata hivyo, Baraza la Serikali ya Mpito (NTC), limekuwa likisisitiza kwamba alijeruhiwa wakati wa mapambano makali ya risasi baina ya wafuasi wake waliokuwa wakimlinda na wapiganaji waliokuwa wakimpinga, lakini baadhi ya mashuhuda wamekuwa wakieleza kuwa aliuawa baada ya kukamatwa.

Mmoja wa makamanda wa jeshi mjini Misratah, ambako ndiko mwili wake ulikopelekwa alisema hawakuwa na la kufanya, morali ya vijana wao iliwazidi nguvu.

“Tulitaka kuhakikisha kuwa anakamatwa na kufikishwa kunakohusika akiwa hai. Lakini kutokana na vijana tuliokuwa nao, mambo yaligeuka, walituzidi nguvu,” alisema.

Taarifa nyingine zinasema Kanali Gaddafi alikuwa na utajiri unaozidi dola200 bilioni za Marekani ikiwa katika fedha taslimu na dhahabu uliofichwa katika akaunti za siri maeneo mbalimbali duniani.

Taarifa zilizopatikana awali wakati vuguvugu la kumwondoa madarakani lilipoanza, zilieleza kwamba amehamishia sehemu kubwa ya utajiri wake nchini Zimbabwe.

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limeeleza kwamba inaaminika Libya inazo zaidi ya tani 140 za dhahabu zilizofichwa nje ya nchi hiyo, nyingi zikiwa zimefichwa kwa kutumia jina la Benki yake Kuu.

Inaaminika kuwa Kanali Gaddafi alichukua kiasi kadhaa cha dhahabu na fedha katika siku zake za mwisho, ili kuzitumia kama sehemu ya makubaliano na wale watakaomkamata.

Utata wa maziko
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Sky News, baada ya kuibuka kwa mvutano kuhusu maziko ya kiongozi huyo wa zamani wa Libya, huenda mwili wake ukakabidhiwa kwa ndugu zake,.

Msemaji wa Mambo ya Nje wa NTC, Ahmed Jibreel alikaririwa na kituo hicho akisema makabidhiano hayo huenda yakafanyika haraka.

Iwapo matatizo hayo yaliyojitokeza na kutoelewana kuhusu suala hilo yasipofikiwa kwa wakati, hali ya amani ya Libya huenda ikawa katika utata zaidi.

“Ninadhani uamuzi tayari umeshafikiwa, ambao ni kuukabidhi mwili wa Gaddafi kwa familia yake ambayo ni pana na iliyotawanyika maeneo mengi.

“Kuna majadiliano ambayo yamefanyika baina ya NTC na watu wa kutoka Sirte, ambako mwili wake huenda ukakabidhiwa. Baadhi ya ndugu zake wako Sirte na wengine katika miji mingine. Tunatarajia hili litafanyika mapema, kama si katika saa chache zijazo, itakuwa katika siku chache zijazo,” alisema Jibreel.

Kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu, mwili huo ulitakiwa kuzikwa katika muda usiozidi saa 24 baada ya kifo chake, lakini sasa tayari umeshafikisha zaidi ya saa 60.

Kanali Gaddafi aliuawa Oktoba 19, mwaka huu baada ya mapambano ya takriban miezi saba na waasi wa nchi hiyo ambao walikuwa wakiungwa mkono na mataifa ya Jumuiya ya Kujihami ya Ulaya Magharibi (Nato), tangu Februari mwaka huu baada ya machafuko katika nchi za Tunisia na kisha Misri.
TATA WATANDA JUU YA SEHEMU WALIPO WAREMBO WALIOKUWA WAKIMLINDA

KANALI Muammar Gaddafi, “Mfalme wa Wafalme wa Afrika” na mtu aliyekuwa na ndoto za kuliunganisha Bara la Afrika, sasa ameyeyuka katika ulimwengu huu, kama mshumaa uliowaka na kuteketea.Ni wazi kwamba mambo mengi aliyoyafanya enzi za utawala wake yaliashiria kuwa alipenda kulijenga jina lake liheshimike ulimwengu mzima.

Lakini kifo chake cha kupigwa na kushambuliwa kama mwizi na taarifa za mazishi yake kuwa ya siri katika kaburi la siri ni hatua nyingine ngumu kwa waliokuwa wakimuamini.

Katika hili, nia hasa ni kujaribu kufuta kabisa historia ya kiongozi huyo wa Libya, nchi inayozalisha mafuta kwa wingi Afrika. Pia kunafuta heshima za kuenziwa kama walivyo viongozi wengine duniani.

Kifo chake hakitofautiani na kilivyokuwa cha kiongozi wa mtandao wa Kigaidi Duniani cha Al-Qaeda, Osama Bin Laden ambaye aliuawa na kikosi cha askari maalumu kutoka Marekani akiwa mafichoni nchini Pakistan na mwili wake kuzikwa kwa siri.

Gaddafi ambaye alizaliwa Juni 7, 1942 aliitawala Libya kwa miaka 42 tangu mwaka 1969, pia aliwahi kunadi wazo lake la kuungunisha nchi za Kiarabu, ambalo lilishindikana.

Hiyo ni hatua moja, wazo hilo lilishindikana baada ya wakuu wa nchi nyingi kudai hatua hiyo ni mapema mno kuichukua, hakusita, akachukua hatua nyingine, kuelekeza nguvu zake katika kujenga Muungano wa Nchi za Afrika (USA).

Wazo hilo pia halikuwa jepesi kukubalika na viongozi wa nchi za Afrika, ambao walisema ni wazo jema, lakini bado linahitaji muda na linaweza kufanikiwa baada tu ya kuweza kuimarisha kwanza jumuiya za kikanda.

Hakusita kutafuta namna nyingine, ambapo aliamua kuwatumia machifu wa kikabila ambao aliweza kuwasaidia kifedha ili wamuunge mkono, kwa kuwatumia hao, aliamini kuwa ataweza kuanzisha ufalme mmoja katika Afrika. 

Hapo ndipo alipojiita “Mfalme wa wafalme wa Afrika” baada ya kuitisha mkutano wa wafalme na machifu wa koo mbalimbali Afrika na katika mkutano huo alioungoza, ndopo akijipa jina hilo.

Kifo cha Gaddafi
Kanali Gaddafi anakuwa kiongozi wa kwanza kuuawa tangu kuanza vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya kiarabu mwanzoni mwa mwaka huu, yaliyowaondoa madarakani Rais Ben Ali wa Tunisia na Hosni Mubarak wa Misri.

Kifo hicho kimetokea ikiwa ni miezi tisa tangu kuanza kwa upinzani mkali dhidi ya Serikali yake Februari, mwaka huu, ambapo aliapa kwamba asingeondoka nchini Libya na kwamba yeye na wafuasi wake wangepambana hadi tone la mwisho la damu.

Kanali Gaddafi alikuwa akisifika kwa ukali wa sauti yake na maneno makali ya kuhamasisha na kueleza misimamo yake katika hotuba zake.

Historia yake
Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hakusita kutumia mbinu za kuhalalisha mashambulizi yake dhidi ya waandamanaji, pale alipogeuza dhana hiyo na kuwaita waasi, kiasha kuapa kuwatafuta wanaompinga nyumba kwa nyumba, mlango kwa mlango.

Kwa mujibu wa taarifa, zaidi ya watu 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya na watu wanaoshirikiana na mtandao wa el Quaeda.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss mwaka 1969, wakati akiwa kwenye matibabu. 

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Alizaliwa katika mji wa Sirte, katika familia ya Mohamed Abdulsalama Abuminiar na mama Aisha Ben Niran. Alijiunga na Jeshi la Libya mwaka 1965.

Alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa mfalme Idris katika utawala wake mwaka 1969 na kuwa mtawala wa Libya akiwa na umri wa miaka 27.

Alikuwa maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.

Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am. Umoja wa Mataifa (UN) ulikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Libya.

Baada ya miezi kadhaa, Serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za Magharibi.

Gaddafi ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar, mtaalam wa siasa za Libya.

Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.

Njama za kimapinduzi
Alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi. Alipata mafunzo nchini Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya. Alipanga mapinduzi Septemba 1, 1969 akiwa katika mji wa Benghazi.

Alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi. Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa uliojumuisha kanuni za Kiislamu na mfumo ulio tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.

Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa akitumia makazi maalum kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.
Hema hilo pia lilitumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo na alikuwa na tabia ya kupepewa kwa jani la tawi la mitende.

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za Bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.
Aliwahi kuvunja na kufuta Wizara za nchi hiyo pamoja na bajeti zao, isipokuwa Wizara chache ikiwemo ya Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.

Vuguvugu la mageuzi

Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu. Vuguvugu la mageuzi dhidi yake lilipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, alitarajia kupata kuungw amkono na nchi marafiki, ikiwemo AU. Hata hivyo, hazikuwa na nguvu na umoja wa kumlinda.

Hali hiyo ilisababisha vikosi vya usalam vya nchi hiyo kuanza kufanya vitendo vya utesaji dhidi ya waandamanaji ikiwepo kutumia helkopta kuwavurumishia mabomu.

Mataifa ya Magharibi yalitumia kauli kuwa wanataka kuzuia utawala wa Gaddafi usiendelee kuwaangamiza wandamanaji ambao wanadai haki yao ya kuupinga utawala wake uliodumu kwa zaidi ya miaka 40.

Baada ya baadhi ya askari kutangaza kujitoa katika jeshi lake na kuanzisha uasi, aliapa kwamba atapambana hadi tone la mwisho la damu litakapomwagika. 

Kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, uliamua utawala wa Gadaffi upigwe marufuku kurusha anga kwenye anga lake ili kuepusha vitendo vya kinyama dhidi ya raia.

Lakini kinyume na uamuzi huo wa UN, mataifa ya Magharibi, yakiwemo Ufaransa, Marekani na Italya yaliendesha operesheni za mashambulizi ya anga kuvunja nguvu za kijeshi za Gaddafi.

Mpango huo ambao ulipingwa vikali na mataifa mengi ya Afrika ulizidi kukolezwa zaidi baada ya baadhi ya mataifa hayo ya magharibi kudaiwa kuwapelekea waasi shehena ya silaha za kivita. 

Vita hiyo ilisonga mbele hadi … walipofanikiwa kuuteka mji mkuu wa Tripoli na kutangaza ushindi japokuwa vikosi vinavyomtii Gaddafi vilibakia katika miji ya Sirte na Minsrata.

Mapambano yaliyondeshwa na waasi hao ambao wanaongozwa na Baraza la Muda la Kitaifa (NTC) yaliweza kukomboa miji hiyo wakimalizia na Sirte, ambao kiongozi huyo
aliuawa. 

Wako wapi mabinti waliomlinda Gaddafi?
SI jambo la kawaida hasa kwa nchi ya Kiarabu, lakini hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Kanali Muammar al- Gaddafi alipokuwa madarakani.Yeye alikuwa kiongozi pekee duniani aliyekuwa akilindwa na kundi kubwa la wasichana warembo wasiopungua 40.
Warembo hao, 'Amazon Bodyguards' ambao walisafiri naye hata katika safari za nje ya Libya hawajulikani walipo sasa tangu utawala wake uliposambaratika.

Kumekuwa na uvumi kwamba baadhi ya wasichana hao ambao wakati wa utawala wa Kanali Gaddafi walitunzwa vizuri, walibakwa huku wengine wakiikimbia nchi hiyo na kwenda uhamishoni Italia.

Lakini, wasichana hao wanasemekana kuwa walishiriki kwa mara ya mwisho bega kwa bega na askari wengine mwezi Agosti wakati mji wa Tripoli ulipotekwa na waasi. 

Ni vigumu kueleza kigezo halisi kilichotumika katika kuwachagua wasichana hao kwa kazi ya kumlinda Gaddafi.

Inasemekana kuwa Gaddafi mwenyewe ndiye aliyekuwa na jukumu hilo la kuwachagua wakiwa bado na umri mdogo, sifa na kigezo kikiwa usafi wa mwili, ambako ilikuwa lazima kwa msichana huyo awe bikira. 

Baada ya uteuzi huo, inaelezwa kuwa wasichana wale walikabidhiwa kwa Gaddafi, kisha kupewa mafunzo mahsusi yakiwamo ya viungo na matumizi ya silaha za aina mbalimbali, yote yakifanyika katika chuo maalumu, kisha kuingizwa katika kikosi hiki maalum.

Siku zote wasichana wale walionekana wakivaa mavazi ya kijeshi ya rangi ya khaki au suti maalum na kofia nyekundu. Pia walionekana wakiwa wamepaka rangi kucha zao na vidani vya thamani hata wakati wakiwa kazini.
Wakati wote wa utawala wake, Gaddafi alisafiri na Amazon Guards, ambao walikuwa wa rangi tofauti kwa idadi ya wasichana 15 au zaidi kwa safari moja. 

Kitu cha kushangaza ni wakati akiwa ziarani, ilikuwa nadra kuwaona wakiwa wamejipanga kando ya kiongozi wao wakati akihutubia kama ilivyo kawaida kwa walinzi wengine wa viongozi. 

Ili kuonyesha ukamavu wao, mmoja wao aliuawa mjini Tripoli wakati msafara wa Gaddafi uliposhambuliwa naye mrembo yule kujitosa barabarani akikabiliana na risasi zilizokuwa zikielekezwa kwao.

Asili ya jina Amazon
Jina hilo lilibuniwa na waadishi wa habari wa nchi za magharibi.Wengine waliwaita 'Watawa wa Kimapinduzi', au 'Watawa Kijani', ambao walikuwa wameteuliwa kwa kazi maalum ya kumlinda Kanali Muammar al-Gaddafi.

Kundi hili liliundwa miaka ya 1980 baada ya Gaddafi kubadili mfumo wa utawala wake na kuunda Jamhuri ya Kiislamu ya Libya. 

Tofauti na miaka ya '70 ambayo Gaddafi alijulikana kwa kauli zake kali wakati huo ambao aliandika kitabu maarufu 'Green Book' alieleza kuwa alibaini kuwa wanawake wana jukumu kubwa zaidi ya kutunza nyumba na watoto.

Imani yake (Gaddafi) inasemekana ni kuamini kuwa wanawake wangeweweza kuwa walinzi wake kwani isingekuwa rahisi kwa mwanaume wa Kiarabu kumpiga risasi na kumuua mwanamke. 

Wengine wamekuwa wakidai kuwa mapenzi ya Gaddafi kuwa karibu na wanawake warembo ndiyo yaliyomfanya aamini katika ulinzi ule wa Amazon Guards.

Baada ya uteuzi na mafunzo yao ya kijeshi, walikula kiapo cha utii cha kutunza usafi wa mwili. Lakini, waliachiwa uhuru wao wa kuishi wapendavyo na kuvaa nguo za kifahari zikiwamo za kutoka Ulaya, kujipamba, kusuka nywele na kuvaa viatu virefu.

Kuna habari kwamba mmoja wa walinzi wale aliuawa Juni mwaka 1998, wengine saba wakijeruhiwa baada ya wanaharakati wa Kiarabu kuvamia msafara mrefu wa magari wa kiongozi huyo wa zamani wa Libya. 

Inadaiwa kwamba mlinzi huyo aliyefahamika kwa jina la Aisha, ndiye alikuwa kipenzi cha Gaddafi na alifanya hivyo kuzuia risasi zisimpate bosi wake

Mwezi Novemba 2006, wakati akiwasili Uwanja wa Ndege wa Abuja, Nigeria, akiwa na ujumbe wa watu 200 wengi wakiwa na silaha nzito, wanausalama wa Nigeria waliingia matatani kwa kujaribu kuwapokonya silaha.

Tukio hilo lilizua mzozo wa kidiplomasia baina ya nchi hiyo na Nigeria. 

Kwa hasira, Gaddafi aliondoka mahali hapo akiashiria kuwa tayari kutembea umbali wa kilometa 40 hadi mjini kwa miguu, lakini akashauriwa apunguze jazba baada ya Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, aliyekuwa uwanjani hapo kuingilia kati.

Misimamo mingi ya Gaddafi iliashiria kuwa ni mtu asiyependa kudharauliwa bali anayetukuzwa na kuheshimiwa mbele za watu wa nje na ndani ya nchi yake.

Pamoja na hali hiyo, mwisho wake umeonekana ni wa kudharauliwa na hata mazishi yake yamefanyika kama mtu ambaye ni hatari na asiye na heshima kwa wananchi wa Libya.


 CHANZO:Mashirika ya Habari

No comments:

Post a Comment